Balozi wa Papa apongeza Kanisa katika mapambano dhidi ya mila potofu
BALOZI wa
Baba Mtakatifu nchini Askofu Mkuu Marek Solczynski amelishukuru Kanisa Katoliki kwa kuendelea
kutoa elimu juu ya madhara ya mila potofu, hasa ukeketaji wa watoto wa kike,
ndoa za utotoni na ndoa za mitara.
Akizungumza
na Kiongozi mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kichungaji ya siku 8 ndani ya Jimbo Katoliki Musoma
balozi huyo amesema kuwa, kuna baadhi ya
udekano alizotembelea na
amekutana na changamoto kubwa ya kupewa taarifa ya kuwepo kwa vitendo vya
ukeketaji wa watoto wa kike, ndoa za utotoni na ndoa za mitara ambazo zimekuwa
changamoto kubwa kwa wakristo walio wengi hata kushindwa kupata sakramenti
takatifu ya ndoa kutokana na kuwa na wake wengi.
“Nimefika
nimeona mimi mwenyewe kwa macho yangu ,nimesikia kutoka katika taarifa
zilizowasilishwa kwangu na mapadri wa udekano wa Tarime, Rorya na Serengeti.
Awali nilikuwa nasoma kwenye vyombo vya habari ila nimewaona na waamini wetu
hivyo ninalishukuru kanisa kwa kuendelea kupambana na changamoto hizi na Mungu
atawasaidia na sisi tunazidi kuwaombea” amesema balozi huyo.
Naye Askofu
wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila amesema kuwa wanamshukuru
balozi wa Papa kwa kutembelea jimbo hilo na kuonana na waaamini sambamba na
kujionea changamoto ambazo wanakumbana nazo katika uinjilishaji.
Mkuu wa
udekano wa Serengeti ambapo ndipo alipohitimishia ziara yake ya kichungaji na
kupata fursa ya kutembelea hifadhi ya wanyama ya Serengeti na kubariki hoteli
na waaamini wanaoishi ndani ya hifadhi,Padri Medard Chegere amesema kuwa ujio wa Balozi huyo umewaimarisha zaidi
waamini kiroho, kwani viongozi hao wanapofika
katika maeneo yao ya kichungaji wanawasaidia kuinuka kiimani zaidi.
Padri Chegere
amesema kuwa waamini wanapaswa kuishi kwa kufuata mafundisho ya Kristo hivyo
kufuata msingi ya imani kutokana na mafundisho ya ubatizo.
Katika hatua
nyingine balozi huyo amewaomba wananchi
wa Wilaya ya Tarime kuhakikisha amani upendo na mshikamano uliopo unaendelea
kudumu ili kizazi kijacho kiweze kufurahia matunda ya amani hiyo.
Balozi huyo
ameyasema hayo alipofanya ziara ya kichungaji katika Parokia ya Tarime na
kuweka jiwe na msingi katika ujenzi wa kanisa jipya ambapo alifurahishwa na
mapokezi ya viongozi mbalimbali wa dini, serikali na waamini wa parokia hiyo na
kusema kuwa ushirikiano huo udumu milele.
“Umoja
mliouonyesha ni dhahiri kuwa kuna amani ya kutosha miongoni mwenu, bila kujali
itikadi ya dini. Nawaomba ushirikiano huu uendelee hata katika masuala mengine
ya maendeleo ndani ya wilaya yenu, ili watoto wadogo hawa watakapokuwa wakubwa
waweze kufurahia matunda ya amani hii” amesema Askofu Mkuu Marek.
Kwa upande
wake Askofu Msonganzila amesema kuwa Kanisa limekuwa bega kwa bega na serikali
katika kuhamasisha umuhimu wa uwepo wa amani miongoni mwao, na hata inapotokea
kuna viashiria vya uvunjivu wa amani wamekuwa wakitumia muda mwingi kuhubiri
amani na upendo na hata namna ya kupinga mila na desturi potofu, hususani za ukeketaji kwa watoto wa kike na
ukatili wa kijinsia pamoja na nyumba ntobhu ili kudumisha amani.
Mkuu wa
Wilaya ya Tarime Glorius Luoga amesema
kuwa kanisa lina mchango mkubwa katika kuhamasisha amani na kwa kudhihirisha
hilo ndiyo maana hata katika mapokezi ya balozi kanisa limealika hata viongozi
mbalimbali wa madhehebu mengine hii yote
ni kuonyesha ni kwa jinsi gani kanisa lilivyo na ushirikiano.
“Naomba
niseme ukweli viongozi hawa wa dini kushiriki katika mapokezi inaonyesha upendo
wa kweli kwani wengine wangeweza kukataa, lakini sisi wana Tarime tumekuwa
tukifanya kazi kwa kushirikiana pamoja na ndiyo maana amani sasa hivi
imetawala, na hata inapotokea dalili za uvunjivu wa amani mimi nikiwa
mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama tumekuwa tukishirikiana na viongozi
wa dini kukemea kwa nguvu zote uvunjifu huo” amesema Luoga.
Comments
Post a Comment