Vyombo vya Kanisa vyatakiwa kuzipa kipaumbele habari za Covid-19

KATIKA kukabilianana Covid-19, vyomba vya habari vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki, vimetakiwa kuzipa kipaumbele habari zinazohusiana na mapambano dhidi ya virusi vya corona husani zile zinazotia matumaini, kuondoa hofu na woga kwa wananchi.
Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Flavian Kasala, katika mahojiano Maalum na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza hilo, yaliyofanyika katikati ya juma jijini Dodoma. Askofu Kasala amehimza vyombo hivyo kutumia hata lugha za asili pale inapobidi ili kuhakikisha ujumbe unaeleweka kwa makundi yote ndani ya jamii.
“Ni kweli lazima tuwe na mashaka, lakini mashaka haya yanatakiwa kuwa yenye matumaini…kumbe vyombo vyetu virudishe hayo matumaini kwamba binadamu anaweza kupigana vita na kushinda na hili ndilo wazo letu kubwa,” amesema.
Pia ametoa wito kwa vyombo hivyo vya habari, kuhakikisha vinautumia ulivyo ujumbe wa TEC kuhusu ugonjwa huo wa Corona hasa kwa kuendana na mazingira halisi ya eneo husika, ili kuufanya ueleweke kwa kila mwananchi ndani ya jamii ambapo amependekeza kutumia hata lugha ya asili ikibidi ili kufikia lengo hili.
“Sasa vyombo vya Kanisa Katoliki ikiwemo TvTumaini, radio zaidi ya 15 na magazeti vina uwezo kabisa wa kuchukua ujumbe wa corona ambao pengine umeandikwa kwenye lugha ngumu ya kitaalam na kuulainisha, ukafikia watu kwanza kwa hali yao, umri wao, na pengine hata mazingira yao na hata kwa lugha zao za asili … kwa sababu corona haichagui na si kwamba watu wote wanaelewa Kiswahili fasaha kwa asilimia 100, lakini ujumbe utaeleweka zaidi na mtu unapozungumzwa katika mila na desturi yake,” amesisitiza.
Upande wa radio na televisheni, Mhashamu Kasala amesema ni vyema kama vyombo hivyo vitatoa ujumbe wa corana kabla na wakati wa habari ama vipindi vingine, kwa kuweka manani kwamba kila mwanadamu ana hulka ya kupenda kitu fulani, hivyo kupitia vipindi hivi atapata cha kujifunza juu ya changamoto hii iliyoukumba ulimwengu.
“Kila mwanadamu ana kitu anachokipendelea…kuna anayependa muziki, kuna anayependa nyimbo za dini na mengine mengi, hivyo kuhakikisha kila mtu anaupata ujumbe huu, ni vyema ukawa unarudiwa mara kwa mara yaani mwanzoni mwa kipindi, katikati na hata kama ni nyimbo ama muziki basi kila baada ya wimbo mmoja mnaweka kibwagizo ama tangazo kuhusu corona,” ameeleza Askofu Kassala.
Upande wa magazeti ya Kanisa hilo, Makamu wa Rais huyo wa TEC, ameyataka kuhakikisha yanatoa habari yenye kubeba ujumbe wa corona na kwamba ujumbe huo hauna budi kuwekwa kurasa za mbele ili uweze kuonekana kwa watu mbalimbali, wakiwemo wale wanaonunua na wasio wanunuzi.
“Habari ziwe kurasa zambele ili hata wale wasionunua lakini wanapita kwenye meza yalipotandazwa magazeti hayo, basi waanze kwanza kosoma habari za corona …yaani katika pitapita yao na kusoma vichwa vya habari vya magazeti, basi wakutane na vichwa vya habari vinavyohusiana na ugonjwa wa corona,” amesema.
Miongoni mwa vyombo hivyo vya Kanisa upande wa radio na majimbo husika yakiwa kwenye mabano ni pamoja na Radio Ukweli (Morogoro), Radio Mwangaza (Dodoma), Radio Fadhila (Tunduru-Masasi), Radio Faraja (Shinyanga), Radio Chemchem (Sumbawanga), Radio Huruma (Tanga), Radio Mbiu (Bukoba), Radio Tumaini (Dar es Salaama), Radio Kwizera (Tulenge-Ngara), Radio Habari Njema (Mbulu), Radio Taa Bora (Tabora), Radio Hekima (Mbinga) na Radio Maria Tanzania.

Upandewa Magazeti ni KIONGOZI (Baraza la Maaskofu-TEC) na TumainiLetu (Dar es Salaam) huku upande wa televisheni kanisa hilo linajivunia TV Tumaini (Dar es Salaam)

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU