Waandishi wa habari watumie takwimu kutoa taarifa-Padri Kitima






Julieth Muunga na  Rodrick Minja, Dar
Wanahabari   wa   Vyombo   vya   Habari   vya   kijamii   nchini   wametakiwa kufanya utafiti wa kutosha katika habari wanazoandika kwa kutumia na takwimu sahihi ili kuleta maendeleo katika jamii.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania TEC, Padri Dakta Charles Kitima wakati akifungua mafunzo ya Siku kumi ya Utafiti kwa Vyombo vya Habari vya Kijamii yanayofanyika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini jijini Dar es Salaam.
Padri   Dakta   Kitima   amesema   kuwa   mwanahabari   mzuri   ni   yule anayefanya   utafiti   wa   kina     na   kwa   kupitia   kazi   zao   mafunzo hayo yatawasaidia   kuimarisha uzoefu na maarifa na kuleta maendeleo kwa Kanisa  na jamii kwa ujumla.
“Wanahabari wengi wa vyombo vya habari vya Kanisa wamekuwa hawajui kufanya utatifi na hawatumii takwimu sahihi wakati wanaandika habari kwenye vyombo vyao vya habari hivyo mafunzo haya nataka yawasaidie ili muweze kuandika habari zenye utafiti na takwimu sahihi ili kulisaidia kanisa na waamini wake” amesema.
Amesema   pia   ni         wakati   wao   kuhakikisha   wanatumia   vizuri   elimu wanayoipata ili waitumie katika uinjilishaji   na jamii lakini wahakikishe wanasaidia kupitia vyombo vyao vya habari     kujenga Umoja na Amani duniani.
Padri Kitima alisema kuwa washiriki wanapaswa kutumia fursa hiyo ya mafunzo hayo vema ili kuhabarisha vema taifa la mungu na kuwapatia mwanga kwa vile ambavyo hawavijui.
“Mwaka huu Kanisa linaadhimisha kilele cha miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, tumieni vyombo venu vya habari kuhakiksiha kuwa mnahabarisha jamii ni nini kimefanyika tokea wamisionari wa kwanza kufika hapa nchini Tanzania na ni mafanikio mangapi yamepatikana tangu wamisionari hao wafike Tanzania” ameongeza Dokta Kitima.
Aidha amesema kuwa tangu mmisionari wa kwanza kufika Tanzania Bara na kuanza uinjilishaji  wananchi wengi wamepata mafanikio katika Nyanja mbalimbali zikiwemo za elimu, afya, maji, kilimo na huduma nyinginezo kwa ajili ya jamii mahalia.
Ameeleza kuwa wakati huu kuelekea  Maadhimisho ya  Kilele cha Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania sambamba na uanzishwaji wa elimu  na huduma nyingine za kijamii, jamii itambue kuwa wamisionari wa kwanza walitumia vitabu   na   magazeti   ambayo   yalikuwa   yakifika   vijijini   hivyo wahakikishe wanaandika habari za kina ili wasaidie watu kuondokana  na umaskini na kujenga uadilifu katika jamii.
Awali Mkurugenzi wa Uchumi Endelevu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC  Meclina Kasasi amesema kuwa mafunzo haya yatawasaidia washiriki kuandika habari zilizofanyiwa utafiti wa kina  na kuhakikisha kuwa habari zinazoandikwa zinakuwa na takwimu nzuri.
“Ni matumiani yangu kuwa mtakayofundishwa mtayafanyia kazi ili kutoa mabadiliko chanya kwenye vituo vyenu vya kazi” ameongeza  Kasasi.
 Amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kujua wasikilizaji wanataka nini na kwa wakati gani hivyo ni jukumu la kila kituo kutekeleza kwa vitendo mawazo ya wasikilizaji wao.
Pia amewataka waandishi wanaoshiriki kuhakikisha hawatumii takwimu ambazo ni za kutengenezwa na sio zilizokusanywa kwa weledi  na utaalamu  wa kutosha.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye pia ni  Mkurugenzi wa Matangazo Radio Mbiu Bukoba, Padri Kagashe Katunzi amesema ameyafurahia sana na anawashukuru waandaji wake maana yanawawezesha kung’amua masuala mbalimbali kuhusiana na tafiti za wasikilizaji kwani watajua  wasikilizaji wanataka nini kitu ambacho kitawasaidia kuboresha maudhui  ya vipindi vya redio na televisheni na namna ya kuviwasilisha kwa wakati husika katika jamii inayowazunguka  huku akiongeza pia ni vyema yawe yanatolewa mara kwa mara kwa wanahabari ili yawasaidie katika taaluma yao.
 Mafunzo hayo ya siku kumi yanashirikisha wanahabari wapatao 25 kutoka  Radio Mbiu Kagera, Radio Huruma Tanga, Radio Ukweli Morogoro , Radio Chemchem Sumbawanga,Radio Mwangaza Dodoma,Radio Tumaini na Televisheni Tumaini Dar es salaam, Radio Sauti Mwanza, Radio Faraja Shinyanga, Radio Habari Njema Mbulu, na Radio Maria Tanzania – Dar es Salaam.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI