Ukuaji uchumi usioheshimu mazingira ni uasi-Ask. Banzi
IMEELEZWA kuwa uharibifu
wa mazingira unaofanywa kwa jina la maendeleo na ukuaji wa uchumi ni uasi sawa
na kuabudu miungu, huku wito ukitolewa kwa kila mwanadamu kusheshimu kazi ya
uumbaji.
Hayo yamesemwa na
Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga Mhashamu Antony Banzi katika Misa Takatifu ya
kuwasimika viongozi wapya wa Shirika la Masista wa mama yetu wa Usambara (COLU)
iliyofanyika katika Makao Makuu ya shirika hilo huko Kwamndolwa, Korogwe.
Akitoa homilia yake
katika misa hiyo Askofu Banzi amesema kuwa mwanadamu amepewa mamlaka juu ya
mazingira huku akitakiwa kutumia zawadi ya akili na utashi katika kuutiisha
ulimwengu na vilivyomo kwa manufaa ya leo na kesho.
“Kuiheshimu dunia ni
moja ya maadili na ni amri ya Mungu. Kuharibu mazingira ni kuabudu miungu.
Tusiitumie dunia kwa fujo kwani atakayeathirika ni mwanadamu mwenyewe.
Tukiitunza nayo itatutunza” amesema Askofu Banzi.
Pia ametaka kuwepo kwa
njia rafiki katika uvuvi na ufugaji wa nyuki, huku akikemea matumizi ya mabomu
na nyavu zisizofaa katika shughuli ya uvuvi, sambamba na uchomaji wa nyuki
wakati wa kurina asali, akisema kuwa njia hizo zinapelekea uharibifu mkubwa wa
mazingira.
Aidha Askofu Banzi
ameweka wazi kuwa matatizo mengi yanayotokea katika jamii husababishwa na
kukosa mahusiano mazuri kati ya mwanadamu na Mungu, ambapo ametaja mwarobaini
wa uharibifu wa mazingira kuwa ni mahusiano mazuri na Mungu pamoja na kuwa na
sheria ambazo msingi wake ni Mungu.
“Tunaiharibu dunia kwa
sababu hatuna mahusiano mazuri na Mungu, hatuna mahusiano mazuri katika jamii
zetu na hata familia zetu” amebainisha.
Wakati huo huo ametoa
rai kwa waamini kutofikiria suala la talaka na badala yake ametaja dawa ya changamoto
za ndoa kuwa ni kujenga mahusiano mazuri na Mungu.
“Talaka ni matokeo ya
kukosa mahusiano mazuri na Mungu. Ukiona mtu anang’ang’ania jambo hilo daima
huwa ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo, jambo la muhimu ni kubaki katika ndoa ama
wito wa utawa” ameongeza.
Uongozi mpya wa COLU
wasimikwa
Katika hatua nyingine
Askofu Banzi amewasimika rasmi viongozi wa Shirika la Masista wa Mama yetu wa
Usambara (COLU) ambapo Mama Mkuu aliyechaguliwa kuongoza masista hao ni Sista
Maria Gaspara Kashamba, ambaye amechaguliwa kwa awamu ya pili mara baada ya
kuwa Mama Mkuu kwa miaka sita iliyopita.
Wengine ni Sista Maria
Focus Mjema aliyechaguliwa kuwa Mama Mkuu msaidizi, Sista Maria Regina, Sista
Maria Vincent na Sista Maria Eveta. Viongozi hao wamekula kiapo mbele ya Askofu
Banzi na waamini waliohudhuria misa hiyo.
Askofu Banzi amesema
kuwa kazi ya Mama Mkuu huyo mpya ni kumiliki, kulinda na kuendeleza utume na
amali zote za shirika hilo hasa kwa kumtanguliza Mungu.
Lijue Shirika la COLU
Shirika la Masista wa
Mama yetu wa Usambara (COLU) lilianzishwa mwaka 1954 katika mkoa wa Tanga
kwenye milima ya Usambara katika Wilaya ya Lushoto na aliyeanzisha shirika ni
Monsinyori Eugeni Arthurs wa Shirika la Mapendo (Mapadri Warosmini).
Monsinyori aliomba
Masista wa Damu Takatifu (CPS) ili walilee shirika hili jipya, ndipo apopewa
Sista Wilibalda Giesbers akishirikiana na Sista Ambrose Mollers ambao walilea
na kuliongoza shirika tangu mwaka huo wa 1954 mpka 1976 walipopokelewa na Sista
Inviolata Mndeme, Mama Mkuu wa kwanza mzalendo.
Walezi hawa waliwapokea
wasichana 12 mwaka 1954 katika shirika. Hadi leo bado wapo masista wawili
waliobaki baada ya wenzao kufariki dunia, nao ni Sista Ancilla Macha na Sista
Bernadetha Massawe.
Shirika hili limekuwa
na watawa wake wafanyakazi katika majimbo ya Tanga, Moshi, Dar es salaam, Same,
Mbulu na Reggio Calabria Italia, ambapo wanatoa huduma za kufundisha dini
maparokiani, kufundisha kwenye shule za chekechea, msingi, sekondari na vyuo.
Pia wanawahudumia wagonjwa mahospitalini,vituo vya afya, zahanati na majumbani.
Comments
Post a Comment