KUYANYAMAZIA MAFUNDISHO YA UONGO NI KUYASHIRIKI

HADI hapo, nilitaka kutoa picha tu ya mafundisho tusiyoyasomea ambayo baadhi yetu wameshajiingiza katika kufundisha. Lakini, kwa nini tunafanya hivyo? Bila shaka, sababu ni tatu: mosi, kutokujua mafundisho ya Kanisa Katoliki ni yapi; pili, kutekwa na vyama vya kitume au vikundi vya dini visivyojali wala kujua mafundisho ya Kanisa Katoliki na tatu, ni tatizo la kumkubali bwana wa pili, ndiye pesa (Mt 6:24).

Mintarafu, kutokujua mafundisho ya Kanisa Katoliki ni yapi ni aibu. Ni aibu kwa padri aliyeandaliwa kuwa mwalimu katika Kanisa kutokujua kitu. Ni aibu kuketishwa chini na kufundishwa mambo batili na kishapo kuinuka yeye mwenyewe kufundisha mambo yasiyo ya Kanisa lake. Tuseme, basi “tumeliwa akili” na wapagani, Wapentekoste, Waislamu na kadhalika.
Inakuaje tuache mafundisho ya kwetu nasi tutumikie dini au makanisa mengine? 

Inakuwaje sisi tulioandaliwa kuwa walimu tugeuzwe kuwa wanafunzi na wale tuliotazamiwa kuwaongoza, yaani walei? Hii ni ajabu ya mwaka!  Kwa aliyeyaona ya Musa haya ndiyo ya Firauni! Tuulizane, je, tutafika? Lakini, ikiwa ni hivi hatuweza kufika salama miaka 300, tusitaje 600 wala 1,000. Pili, kutekwa na vyama vya kitume au vikundi vya dini visivyojali wala kujua mafundisho ya Kanisa Katoliki.

Vyama au vikundi visivyosimama kwenye mafundisho sahihi ya Kanisa Katoliki, hususan, vikiwa na watu maarufu na vikiwa na pesa, vina silika ya kuziba vinywa waliopaswa kuyasimamia mafundisho ya kweli. Huo ni mkasa wa mapadri kuruhusu kufumbwa vinywa kwa pesa. Jambo, hilo ni aibu pia. Haifai padri kunyamazishwa na watu uliopaswa kuwaongoza kuelekea uzima wa milele. Tatu, ni kupotoshwa na sifa binafsi na pesa.

Si siri, tupo wengine ambao tumeshageuka wapenda pesa na “wapiga pesa”. Lakini tukiachilia mafundisho ya uongo yatamalaki kwa sababu ya sisi kupata au kupewa fedha, tumeshakuwa na mabwana wawili, Mungu na pesa, ambao hatutawamudu kuwatumikia kwa moyo sawa. Huu ni mwanzo wa moja kutuponyoka, na naona atakayetuponyoka kwa wepesi ni Mungu. Yohane anasema, tukiupenda ulimwengu hatuwezi kuwa na Mungu (1Yoh 2:15-16).

Mapadri ilitupasa tuwe macho ya waamini
Mapadri,  acha tukumbushane. Ulikuwa ni wajibu wetu kuangalia ubora wa imani yetu na siyo kuachia mafundisho ya Kanisa yakibomolewa. Huko ni sawa na kukata mti tuliokwea wenyewe. Mti utakapoanguka na sisi tutaanguka pia. Kama wadau wa elimu ya imani yetu, ilitupasa kuangalia nani anafundisha katika eneo letu.

Ilitupasa kuangalia nini kinafundishwa katika eneo letu. Ilitupasa kuangalia wapi kinafundishwa kitu cha uongo na ambacho kitafubaisha Kanisa na mustakabali wake. Kanuni ya kimaadili yasema, kuyaachia au kuyanyamazia mafundisho ya uongo ni kuyashiriki. Kwa hiyo, siyo tu dhambi ya kutotimiza wajibu bali ni mchango wa kuukata mti ambao tumeukwea sisi wenyewe.

Kuhamishia mikazo mahali pengine

Si siri, siku hizi, mapadri kadhaa, badala ya imani, tumehamia kwenye kutenda miujiza, karama za kuponya na kunena kwa lugha. Wapi na wapi mikazo hii! Karama zitokazo kwa Roho Mtakatifu hazikamiwi. Huwa zinatolewa na Roho Mtakatifu kama apendavyo mwenyewe, yaani kwa hiyari yake.

Laiti kila padri angegundua karama yake halisi na kuiweka katika matendo, tungepata ufanisi mkubwa zaidi kuliko kumangamanga na kufedheheka kunakobainika sasa. Tatizo hili linachangiwa na kutomakinika kwetu. Lakini, hata kama si kuhamia kwenye karama hizo, karama zilizo bora zaidi ni upendo na unabii (1Kor 14).

Tunageukaje waigaji mambo?
Jinsi tunavyoendelea baadhi yetu ni kana kwamba hakukuwa na haja ya kujifunza lolote Seminarini. Yaani ni kama ilitosha kuwapadrisha watu na wao kufundisha kwa kuwatazamia wengine. Tunaiga wanachofanya makanisa mengine badala ya sisi kudumu katika uelewa wetu halisi mintarafu karama.

Makanisa mengine hawana utulivu wa mafundisho ya sakramenti saba, ndiyo kisa wanahangaika na kukamia karama mbalimbali lakini hasa kufanya miuji na kunena kwa ndimi (lugha). Lakini, haikupasa mambo kuwa hivi katika Kanisa Katoliki. Mambo ya kuponyana yangeliendelezwa vizuri katika mitandao yetu ya zahanati, vituo vya afya na hospitali. Wamisionari walishatuanzia ujenzi wa miundombinu ya matibabu ya kisasa na elimu nzuri.

Lakini, inaonekana kama tunakataa hayo nasi kupeleka yote kwa Roho Mtakatifu. Lakini ingekuwa Roho Mtakatifu atatufanyie yote, Mungu asingelitupa akili na utashi pamoja na neema bali angelitufanya tuishi kwa silika kama wanyama wa kufugwa na hayawani.

Mambo ya kunena kwa lugha, tungeliweza kunena wenyewe na kuwanenesha waamini wetu kwa elimu ya kweli katika mtandao wetu wa elimu tangu chekechea, shule za msingi, shule za sekondari, vyuo  vya ufundi na ualimu pamoja na vyuo vikuu vyetu. Lakini, siku hizi, tunaacha kumakinika na mitandao hii, tunang’ang’aniza moja kwa moja karama za kufanya miujiza, uponyaji na unenaji wa ndimi.
Mimi, sijui ni nani aliyetusadikisha kwamba karama hizi ni bora zaidi kuliko karama zingine? Je, Biblia haijasema upendo ndiyo karama namba wani na inayofuatia ndiyo unabii (1Kor 14)? Kumbe, kung’ang’aniza kwetu karama ambazo hatuna ndiko kunakosababisha tushindwe kufanikisha karama zenyewe.

Injili haitahubirika
Kwa jinsi mapadri tunavyosuasua na imani Katoliki tutasababisha maafa makubwa kwa Injili: haitahubirika. Tunafanya mizaha au tunaachilia mizaha itendeke kwenye matakatifu ya Mungu. Ni mizaha mingi mno:  kulialia, unenaji lugha feki, miujiza feki,  mafuriko ya sala na vitendo vya woga,  “kupiga pesa”,  kujiabisha na kuponzwa kwa wasichana na akinamama wetu, uongo bayana katika uponyaji,  kulegea kwa akinamama wetu, ubishi wa kijinga na kadhalika..

Haya yataugharimu Ukatoliki. Yanawakera sana wanaotutazama. Ukatoliki utageuka kuwa mzaha na dini ya wagonjwa au wajinga tu. Hapo ndipo utume utakapogota. Uinjilishaji hautawezekana kwa sababu watu tunaotaka kuwafikia watakuwa wametutia katika kapu moja na wahuni au wajinga. Watatupuuza na wataupuuza ujumbe wetu. Nahoji.

Hivi tunadhani watu hawafuatilii maendeleo ya Ukatoliki na kugundua jinsi tunavyoudhalilisha? Nimewahi kuwakuta Waislamu wakisema na kushukuru kwamba zamani sana waliwahi kupata matibabu mazuri sana katika hospitali moja iliyokuwa inaendeshwa na “Wakatoliki wale wale wenyewe”. Nilishangaa sana lakini hii ilimaanisha wamegundua siku hizi kuna “Wakatoliki wasio wenyewe”, yaani kuna “Wakatoliki feki”. Kama mambo ndiyo hivi, hii ni balaa kubwa!

Tano, kuwatoa watu hofu kwa kuwahakikishia Yesu yupo nao

Mintarafu kuwatoa watu hofu kwa kuwahakikishia kwamba Yesu pamoja nao, tatizo ni moja: kupamba moto kwa mafundisho ya kutia watu hofu kutoka kwa makanisa mengine na dini zingine wanayodakia Wakristo wetu. Badala ya kuwafikishia watu Habari Njema yenye furaha, waamini siku hizi wanasongwa na mafundisho ya kutisha: majini, laana, kufungwa na mikosi, Shetani na kadhalika. Kituko hiki ni nini?

Wala tusisahau, mtaji wa makanisa mengine na wachungaji wao ni kuwahubiria watu habari za kutisha kusudi watu wakitishika “wawapige pesa”. Natoa mifano. Mafundisho hayo ni hasa, “kuathirika kwa Wakristo na laana”, “kusongwa kwa watu na majini”, “kujiinua kwa Shetani”, “watu kufungwa kwa mikosi na balaa mbalimbali jambo linalohitaji huduma ya kuwafungulia watu vifungo vyao”, “kuathirika kwa watu kwa uchawi na ulozi”, “kusongwa kwa watu na Frimasoni” na kadhalika.
 Kuna mkasa umezuka. Waamini wetu wameyasikia mafundisho haya kutoka kwa makanisa jirani na hivyo na wao kujihisi wanahusika nayo. Kwa namna hiyo wamejinasisha wenyewe kwenye matatizo ambayo hayakuwa lao.

Kumbe, baada ya kujisikia wanahusika nayo wanahisi Kanisa Katoliki “linazubaa” katika kuyashughulikia. Ndipo wanapohangaika na kutaka mapadri wajitose kwa haraka katika kushughulikia hofu hizo. Hapo ndipo, kwa kudhani Kanisa Katoliki linazubaa, baadhi wanapoipokea Karismatiki kama chombo cha kuzishughulikia hofu za namna hiyo.

Mapato yake ni mahangaiko ambayo, mapadre, badala ya kuwatuliza watu na kuwaweka sawa, baadhi wanaunga mkono pamoja na mapendekezo ya “dawa” wanazozianisha “watawa na walei” na wengineo wahangaikao. Huko ndiko kutolewa kwa mapadre kwenye njia nyofu. Kwa kujua au kwa kutokujua, mapadri wengine wametumbukizwa kwenye hofu hizo mno kiasi cha kusahau kabisa elimu yao na teolojia waliyosomea kwa jasho la kutosha.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI