‘Imetosha kujenga makanisa sasa tuhudumie wagonjwa’
Kila jumuiya na Parokia viwe na mfuko wa wagonjwa
Na Pascal Mwanache, Singida
WITO umetolewa kwa waamini katika
ngazi za jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na Parokia kuwa na mfuko wa akiba kwa
ajili ya wagonjwa, kwa kuwa hicho ndicho kipaumbele cha maisha ya mkristo
ambapo kwa sasa mkazo umewekwa zaidi katika shughuli za ujenzi wa makanisa na
miundombinu yake huku wakisahau kuweka akiba ya kujenga miili yao.
Wito huo umetolewa na Askofu wa
Jimbo Katoliki Singida Mhashamu Edward Mapunda wakati wa maadhimisho ya Siku ya
26 ya Wagonjwa Duniani ambayo kitaifa imefanyika katika Hospitali ya Malkia wa
Ulimwengu Puma, Singida. Askofu Mapunda amewataka waamini jimboni humo kuanza
mara moja utaratibu wa kuwa na mfuko wa wagonjwa katika jumuiya na parokia na
kuwa na mguso wa pekee katika kuwajali na kuwahudumia wagonjwa.
“Yesu alipambana na magonjwa
yaliyowaangamiza watu kiroho na kimwili. Hiki kilikuwa kipaumbele cha Yesu na
sasa ndicho kipaumbele cha Kanisa. Kwa njia za huduma ya afya na sakramenti
mbalimbali za Kanisa watu wanaendelea kutakasika. Hicho kiwe pia kipaumbele cha
jumuiya zetu yaani kuhudumiana kimwili na kiroho. Kwa namna hii wagonjwa
watakuwa na matumaini ndani ya jumuiya na Parokia zetu” ameasa.
Aidha Askofu Mapunda amebainisha
kuwa huduma za afya ni wito mtakatifu kwa kuwa muda unaotumika kuwahudumia
wagonjwa ni muda uliotumika kitakatifu. Ameongeza kuwa kuhudumia wagonjwa ndiyo
dini ya kweli na ibada kwa sababu anayehudumiwa ni Yesu mwenyewe.
“Matendo ya huruma kwa wagonjwa ni
ibada. Ni sehemu ya maisha ya kila siku, hivyo ni matendo endelevu. Familia,
jumuiya ndogo ndogo za kikristo, parokia, jimbo na kanisa kwa ujumla lazima
zijikite katika kuhudumia wagonjwa” ameeleza.
Katika hatua nyingine Askofu Mapunda
ametoa wito kwa viongozi wa kiroho kuwahamasisha waamini kuwa na bima ya afya
ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa huduma kwa wananchi wanaokosa fedha
za matibabu pindi wanapougua.
“Nitafurahi kama jumuiya
itahakikisha kwamba kila mwanajumuiya anakuwa na bima ya afya. Kila tunapoenda
kusali tuulizane kama kila mmoja wetu ana bima ya afya, kama tunavyoulizana
iwapo tumebeba Biblia na rozali” ameongeza.
Mkuu wa Mkoa wa Singida aliomba
Kanisa
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi ameliomba Kanisa Katoliki Jimbo la Singida
lifikirie kuwa na kiwanda cha kutengeneza maji ya dripu ikiwezekana ndani ya mwaka
huu, akisema kuwa Bikira Maria ana makusudi ndani ya Singida kuwe na huduma
pekee kwa ajili ya manufaa ya wananchi wote.
Pia amewaomba viongozi hao wa dini
kuomba ili taifa liondokane na wagonjwa wasababishi wa magonjwa kama vile
ubinafsi, rushwa, uvivu, wizi, uzembe kukosa uaminifu na uadilifu.
“Yasipoondoka haya tutafungua
hospitali nyingi. Mtu anayeendekeza rushwa kwa mfano, atachelewesha haki,
atapindisha sheria na kusababisha watu kuugua” ameeleza.
Aidha Dkt. Nchimbi amekiri kuwa
Kanisa ni mkono wa serikali katika utoaji huduma za afya kwa kuwa wadau wakubwa
wa utendaji wa serikali, huku wakitenda kiaminifu na hata kuwa darasa kwa
wengine. Ametoa wito kwa wahudumu wa afya katika hospitali za serikali mkoani
humo kuwapa ruhusa wagonjwa wanaohitaji huduma za CT Scan ili wakazipate katika
Hospitali ya Mt. Gaspar iliyoko Itigi.
“Nataka niwaeleze kuwa mkoa wa
Singida katika Hospitali ya Mtakatifu Gaspar Itigi kuna huduma ya CT Scan
nzuri, bora na ya kiwango cha kimataifa ambayo hatujaitumia vizuri. Hospitali
za serikali msiwacheleweshe wanaohitaji huduma ya CT Scan. Tukiri tu kuwa
tumetindikiwa, kwa hiyo elekezeni mara moja mtu akapatehuduma pale Mt. Gaspar
Itigi. Hapa Puma pia kuna huduma nzuri za tiba ya mifupa. Kuna madaktari bingwa
kutoka Ujerumani, tutumie fursa hii bila kuchelewa” ameongeza.
Dkt Nchimbi agawa Rozari 700 kwa
wagonjwa
Katika kuadhimisha siku hiyo ya
wagonjwa waamini waliohudhuria walipata fursa ya kuwatembelea wagonjwa
waliolazwa katika Hospitali ya Malkia wa ulimwengu Puma na kuwafariji kwa
zawadi na sala zao, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi alikuwa
kivutio kwa wagonjwa hao na waamini.
Kama ilivyo ada yake kila
alipowasalimu wagonjwa, aliwahoji iwapo ni wakristo na iwapo wanahitaji rozari,
na pindi wanapokubali basi yeye mwenyewe huwavalisha rozari hizo pamoja na
kuwapatia zawadi nyingine.
Vyombo vya habari vya Kanisa
vyatajwa kuwa faraja ya wagonjwa
Kiongozi lilifanya mahojiano na
baadhi ya wagonjwa ambapo wengi wamekiri kuwa vyombo vya habari vya Kanisa
Katoliki vimekuwa faraja kwao hasa katika kufuatilia yanayojiri ndani ya
Kanisa, kufuatilia Misa Takatifu na kusoma tafakari.
“Ndiyo ninasoma gazeti la Kiongozi
hasa tafakari za kila jumapili, na hata ninaposhindwa kwenda kanisani
nafarijika kusikiliza Redio Maria” anaeleza Lukas Mbingu aliyelezwa hospitalini
hapo.
Kutoka chumba cha habari
Ili kuwafikia na kuwainjilisha
wagonjwa na wenye uhitaji zaidi vyombo vya habari vya kanisa vinategemea
uwezeshwaji na uungwaji mkono wa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kama
ilivyofanya Kurugenzi ya Uchumi Endelevu ya Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC) ambayo imehakikisha gazeti la kiongozi linawahabarisha waamini
juu ya maadhimisho na matukio ya siku ya wagonjwa 2018.
Comments
Post a Comment