‘Madaktari waende Kenya lakini Tanzania pia ina uhitaji’
“SERIKALI ya Tanzania itafute namna ya kuwaajiri madaktari wake ili
kuziba pengo kubwa la upungufu wa madaktari nchini.”
Hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara Mhashamu Severine Niwe-Mugizi wakati akizungumza na
Gazeti Kiongozi kuhusu maamuzi ya Serikali kutuma madaktari wake nchini Kenya.
Askofu Niwe-Mugizi japokuwa hajapinga uamuzi huo lakini amesema lazima
serikali iangalie uhitaji wa madaktari katika hospitali na vituo vyote vya afya
nchini hususani majimbo yaliyoko pembezoni mwa nchi.
“Sina pingamizi juu ya hilo kwani watu wa Kenya wanaumia kwa sababu
hawana madaktari wa kuwatibu, lakini ninachotaka tukiangalie ni usalama wa
madaktari wetu.
Ikumbukwe kuwa, Chama cha Madaktari Kenya kina mgogoro na serikali hivyo
badala ya kusuluhisha tatizo hilo wanaamua waiingize Tanzania. Je, Chama hicho
cha Madaktari Kenya hakitaiona Tanzania kuwa ni wasaliti? Pili Kenya ina
changamoto za kiusalama kwani mara nyingi wanavamiwa na Al shabaab. Tatu muundo
wa ajira zao upoje? Je, tukiwapeleka ndilo suluhisho?,” amehoji Askofu
Niwe-Mugizi.
Ameiasa Serikali kuwa makini kutoiingiza nchi kwenye matatizo pia
kuangalia matatizo ya nchi yao kwanza kabla ya kusaidia mataifa ya nje.
Kwa upande wake Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu
Methodius Kilaini amesema kuwa, tatizo la Kenya linawapa fursa watanzania
kupata ajira ingawa haijaeleweka kuhusu muundo wa mikataba yao na kuwa itakuwa
mikataba ya aina gani.
“Tanzania imekuwa na vyuo vingi vya Afya, imezalisha madaktari wengi
ingawa hatuwezi kuwaajiri wote. Mimi mwenyewe inawezekana kwenye Jimbo kuna
hospitali na vituo mbalimbali vya afya
lakini hatuwezi kuwaajiri wote. Hivyo badala ya kurandaranda na
kulalamika mitaani watumie fursa ya kwenda huko kufanya kazi.
Hii ni kawaida nchi moja kupeleka madaktari ama wafanyakazi wake nchi za
nje kufanya kazi. India ina madaktari wengi, Ufilipino pia na wengine lakini
wamewatawanya kwenye nchi mbalimbali ili kuingiza pato la nchi na kutatua
tatizo la ajira. Hivyo, kama kuna makubaliano yanayoeleweka, watapata huduma
zote za msingi hususani usalama waende wakaokoe watu wanaoumia, wanaougua bila
kupata matibabu,” amesema Askofu Kilaini.
Hali hii inafuatia makubaliano kati ya serikali ya Tanzania na Kenya
mwishoni mwa wiki ambapo madaktari wapatao 500 watapata ajira nchini Kenya.
Kenya imeahidi kuwa itaendelea kuwasaka madaktari zaidi kutoka mataifa
mengine Afrika ili kufanikisha huduma bora. Sekta ya afya nchini humo
iliathirika zaidi baada ya madaktari kugoma kwa siku mia moja na kufifisha
utoaji wa huduma za afya nchini humo.
Madaktari walioomba nafasi za kwenda nchini Kenya mpaka sasa ni zaidi ya
150.
Comments
Post a Comment