‘Huwezi kutenganisha ukombozi wa Tanzania na Ukristo’
IMEELEZWA kuwa ujio wa
wamisionari wa kwanza Tanzania Bara ndiyo ulikuwa mwanzo wa safari ya ukombozi
na mapinduzi katika nyanja za elimu, afya na fikra nchini Tanzania.
Hayo yamebainishwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Same Mhashamu Rogath
Kimaryo katika Misa Takatifu ya uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 150 ya
uinjilishaji na elimu Bagamoyo, ambapo amesema kuwa licha ya kufanya kazi za
uinjilishaji hapa nchini wamisionari ndiyo waliokuwa chimbuko la wasomi wa
kwanza nchini.
Askofu Kimaryo ameeleza kuwa nguvu hiyo ya Kanisa Katoliki nchini katika
kuhudumia jamii bila ubaguzi ndiyo chimbuko la mafanikio ya utume wake hapa
nchini.
“Wamisionari walipofika Bagamoyo waliwakomboa watumwa, wakawaweka katika
kijiji huru cha Mariani (Marian Village), hapo wakafungua shule wakaanza
kuwafundisha watumwa hao kusoma. Wasomi wa kwanza Tanzania walikuwa ni hawa
watumwa waliokombolewa Bagamoyo mwaka 1868” ameeleza Askofu Kimaryo.
Ameongeza kuwa kazi hiyo kubwa iliyofanywa na wamisionari wa kwanza
ndiyo inayoendelezwa hata hivi leo, huku akibainisha kuwa uwepo wa shule nyingi
zinazoendeshwa na kumilikiwa na kanisa Katoliki nchini ni chachu katika
kuelimisha taifa.
“Kanisa siyo tajiri. Kanisa linaratibisha vitu vizuri tena kwa majitoleo
makubwa. Umisionari ni unyenyekevu, ndivyo Kanisa linavyofanya kazi yake; kwa
unyenyekevu, bila majivuno huku likiruhusu mpango wa Mungu” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Askofu Kimaryo ambaye aliongoza Misa hiyo ya uzinduzi
wa jubilee, ameonya kuwa ni lazima watanzania watunze maeneo ya kihistoria na
kuwataka wanasiasa wasisababishe kupotea kwa historia hiyo.
Ametahadharisha kuwa Bandari ya Bagamoyo ni ya kihistoria na inapaswa
ibaki kama sehemu ya historia, na endapo kuna aina yoyote ya upanuzi litafutwe
eneo pembeni yake ili eneo hilo libaki katika kumbumbuku ya historia.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor
Mkude amewataka waamini wa Bagamoyo kuongeza kasi ya kutafuta utakatifu hasa katika
kipindi hiki cha mwaka wa jubilei. Ametoa rai kwa wazazi kuwa mfano wa kuigwa
katika malezi ya watoto wao kwa kuishi na kuwafundisha katekesi.
“Wazazi ishini kwa mfano ili watoto waige na wajifunze sala kutoka
kwenu. Tusingoje watoto wafike darasa la pili ndipo tuanze kuwafundisha
katekesi, elimu inaanza mapema lakini katekesi ianze mapema zaidi. Kila mmoja
atimize wajibu wake, pamoja na Kristo tutafanikisha” ameeleza.
Comments
Post a Comment