PICHA 16 ZA SIKUKUU YA MAPADRI WA JIMBO KUU DAR ES SALAAM LEO
Mapadri wanaohudumu katika jimbo Kuu Dar es Salaam
wameadhimisha Sikukuu yao kwa Ibada ya Misa Takatifu ya Kubariki Mafuta
iliyofanyika Katika Kanisa Kuu la Mt. Yosefu jimboni humo.
Adhimisho hilo limeongozwa na Mhashamu Askofu Eusebius
Nzigilwa, Askofu Msaidizi wa jimbo hilo leo Jumanne, siku iliyotengwa na jimbo
kuwakutanisha Mapadri wote kusherehekea sikukuu yao iliyowekwa na Yesu Kristu
siku ya Alhamisi Kuu ambapo aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na
Sakramenti ya Upadri.
Pamoja na mambo mengine Mhashamu Askofu Nzigilwa amewaongoza
mapadri kubariki mafuta ambayo hutumika katika maadhimisho ya Sakramenti
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mafuta ya Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa, Mafuta
matakatifu ya Krisma na Mafuta ya Wakatekumeni.
Aidha mapadri wamerudia ahadi zao za upadri, tendo ambalo
limeongozwa na Mwadhama Polycap Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa jimbo hilo la
Dar es Salaam.
Sikukuu ya Mapadri huadhimishwa kila Alhamisi Kuu
Ulimwenguni kote ila kutokana na mahitaji Jimbo Kuu Dar es Salaam liliweka
utaratibu wa kuadhimisha sikukuu hiyo siku ya jumanne lengo likiwa ni
kuwawezesha Mapadri kutoa huduma katika parokia zao siku ya Alhamisi Kuu.
Sikukuu hiyo imesherehekewa na mapadri zaidi ya 300.
Adeline Berchimance
Comments
Post a Comment