Wanaohitimu elimu ya juu watakiwa kutatua changamoto za wananchi
ASkofu Mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo
Kuu Katoliki Tabora amewaasa wahitimu wa
Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora, (AMUCTA) kutumia elimu
waliyoipata katika kutatua matatizo ya wananchi wa Mkoa wa Tabora na Tanzania
nzima.
Rai hiyo
imetolewa hivi karibuni katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyoadhimishwa
katika Kanisa la Chuo hicho ambapo
Askofu amesema elimu ina lengo la kumsaidia mwanadamu amudu mazingira yake .
Elimu ni
ufunguo, elimu ni mwanga unaomsaidia mwanadamu kuwa mstaarabu na kupeleka
ustaarabu huo kwa wengine katika jamii anayokuwemo na si kitu cha kumpatia
mwanadamu kiburi na majivuno.
Askofu
Ruzoka amesema, elimu inamsaidia mwanadamu kuwa bora zaidi katika kueleza mambo
kwa ufasaha zaidi kwani anakuwa na ufahamu mkubwa zaidi tofauti na hapo awali,
elimu hiyo inaongeza ufanisi katika utendaji wake wa kila siku.
Amewataka
wahitimu hao kumtanguliza Mungu zaidi ili waweze kutafuta Hekima katika Ukweli,
“seek Wisdom in truth” ambayo ndiyo kauli mbiu ya Chuo cha “AMUCTA.”
Tukumbuke
kuwa wote tunaingia katika ulimwengu huu na kuondoka kwa namna moja. “Je
utakapoondoka utakumbukwa kwa lipi?”. Askofu Mkuu aliuliza.
Aidha
Askofu Mkuu Ruzoka amesema kila mhitimu ameiva, hivyo ana kila sifa ya kuwa
kiongozi katika jamii ya watu atakaokutana nao, hivyo tumieni elimu mliyoipata
kwa faida ya jamii nzima na si kwa maslahi binafsi.
Askofu
Mkuu Ruzoka amewasisitiza wahitimu wote kutumia elimu waliyopata kupambanua
mema na mabaya.
Aidha
Askofu Mkuu Ruzoka amewakumbusha wahitimu wote kuwa na moyo wa shukrani kwa
Mungu na wazazi au walezi kwa michango yao mbalimbali iliyowawezesha kufikia hatua hiyo kubwa katika uwanja wa
elimu kwani moyo usio na shukrani hukausha meema yote.
Askofu
Mkuu Ruzoka amewasihi wahitimu wote kujiendeleza katika uwanja huo wa elimu ili
kwenda sambamba na ulimwengu unaokwenda kasi
hasa katika mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ili wasibaki nyuma ya
wakati.
Pia
amesema elimu mliyoipata iwaongezee hamu ya kulitumikia Taifa letu na Kanisa
zima , daima tukumbuke hapa duniani tunapita na elimu yetu pia na vivuli vyetu,
ipo siku itatubidi kutoa hesabu ya maisha yetu, vyema tuishi kwa upendo na watu
wote.
Wito
ulitolewa pia kwa wanafunzi wote kuweka bidii katika masomo ili kuweza kufikia
hatua ya kuhitimu, “komaeni katika kusoma yanawezekana” Askofu Mkuu amesema.
Aidha
amesema Digrii mlizopata zitumieni katika kuhudumia watu, nasiyo kupamba katika
mitandao ya kijamii bali zitumike katika kuboresha maisha yenu na wengine,
mkiwa wabunifu, tayari kujiajiri na kuajiri wengine.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri akizungumza muda mfupi baada ya Misa
Takatifu amewaasa kutumia digri zao kupambana na mazingira na siyo kulalamika
kila kunapokucha, jueni kazi ya elimu ni kumpa uwezo mwanadamu kutafuta fursa
na kuchukua kadri ya mazingira yake.
Aidha
amewaasa wahitimu wote kuwa digrii lazima ilete mabadiliko ya haraka kwa
mhitimu mwenyewe na wale wanaomzunguka katika utendaji wake.
Mh.
Mwanri ameelezea umuhimu wa sekta ya viwanda kwa maendeleo ya kila mtanzania.
Mkuu wa
Mkoa amewapongenza wanatabora hasa kupokea mabadiliko na kupunguza mimba za
utotoni lengo likiwa ni kupata mhitimu wa Shahada ya kwanza kwa kila nyumba ya
mkazi wa Tabora.
Aidha
Mkuu wa Mkoa wa Tabora aliwahimiza wahitimu wote kubuni namna ya kujiajiri na kuwaajiri wengine, ili
kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira linalolikumba Taifa letu na mataifa
mengine duniani.
Pia aliwahimiza wahitimu wote kukumbuka
kurudisha mikopo waliyokopeshwa na Serikali ili kuongeza uwezo serikalini wa
kukopesha wengine. Nendeni mkawe mabarozi wazuri wa chuo cha “AMUCATA”. Haya ni
mahafari ya saba tangu Chuo Kianzishwe.
Comments
Post a Comment