Askofu Dallu akemea uchumba sugu
WAamini wameaswa kuachana na tabia ya kuishi uchumba sugu bila kufunga ndoa.
Badala yake wafunge ndoa ili wapate kupokea sakramenti mbalimbali katika
kanisa.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu Mkuu Damian Dallu
wa jimbo Kuu Katoliki Songea, wakati
akihubiri katika Misa Takatifu ya jubilee ya miaka hamsini ya Parokia ya Mtakatifu Martin wa Tur
Mpandangindo iliyopo katika jimbo Kuu Katoliki Songea.
Askofu Dallu amesema kuwa, suala la uchumba sugu limekuwa
likijitokeza katika parokia nyingi jimboni Songea na kuhimiza kuwa, waamini
hawana budi kushika amri za Mungu na Kanisa kikamilifu.
Ameongeza kuwa, suala la kutoa zaka kwa waamini ni la
msingi na kwamba waamini waachane na tabia ya kutoa zaka kwa Kanisa wakati
wanapokuwa na majukumu ya kusimamia na kupokea sakramenti tu.
Akizungumzia sherehe ya Jubilei ya miaka 50 ya parokia
hiyo ya Mpandangindo Askofu Dallu amesema , anatoa shukrani kwa uwepo wa
wamisionari Wabenediktini walioleta Imani katika jimbo Kuu Katoliki Songea.
Aidha amewataka
waamini kuzisafisha nafsi na kuishi maisha yanayompendeza Mungu, na kuendelea
kuliishi Neno la Mungu kama walivyofundisha wamisionari hao na kuwataka waamini
kuwa na roho ya huruma, upendo na ukarimu kwa Kanisa zima la Mungu na
kulitegemeza Kanisa.
Askofu Dallu amesema, Yesu Kristo tunakutana naye katika
maisha ya kila siku na kufafanua kuwa
tunakutana na Yesu katika Misa Takatifu, katika Neno la Mungu, katika
Ibada za kuabudu Ekaristi Takatifu.
Aidha katika mafundisho ya katekesi na katika matendo
mema kwa wenzetu kama alivyofanya mtakatifu Martin wa Tur mlinzi wa parokia ya
Mpandangindo ambaye alitoa hata kipande cha nguo yake kwa ajili ya wahitaji.
Parokia ya Mpandangindo kwa sasa inahudumiwa na mapadri
wamisionari wa shirika la Wakarmel ambao hapa nchini Tanzania wapo katika Jimbo
Katoliki Morogoro wapo parokia ya Malolo na Kihonda-, wapo pia Jimbo
Kuu Katoliki Dar es salaam katika parokia ya mtakatifu Peter Claver Mbezi
Luise, Parokia ya Teresia Mtoto Yesu Mbezi Mwisho na parokia ya Malamba ya
Yohane wa Msalaba.
Jimbo Kuu Katoliki
Mbeya wapo katika parokia ya Yakobo Mtume
Uyole, na katika Jimbo Kuu Katoliki Songea Parokia ya Mpandangindo ya Mtakatifu Martin wa Tur.
Comments
Post a Comment