TEC yatoa mafunzo kwa wanawake kuhusu uchumi shirikishi

BAraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC limetoa mafunzo ya siku mbili kwa wanawake  wa kada mbalimbali juu ya uchumi wa soko jamii.
Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia Novemba  15 -16 mwaka huu katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Kurasini jijini Dar es Salaamna kuhudhuriwa na wanawake kutoka majimbo zaidi ya 20 kwa maendeleo endelevu na shirikishi y akiuchumi na kijamii.
Akifungua mafunzo hayo  Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mhasham Prosper Lyimo amewataka wanawake nchini kuitumia vizuri fursa ya mafunzo ya uchumi wa soko jamii shirikishi wanayoyapata ili yawasaidie wao na wengine kujikwamua kiuchumi na kukuza uchumi wa Taifa.
Askofu Lyimo amesema Kanisa lina miradi mingi yenye lengo la kuwasaidia watu wote kwa pamoja wa mjini na vijijini, hivyo amewataka wanawake hao kuyatumia vyema mafunzo wanayoyapata kwa manufaa yao na ya wengine sambamba na kutumia karama walizopewa na Mungu kwa manufaa ya Taifa la Mungu kiujumla.
Amewapongeza wanawake kwa mwitikio chanya waliounonyesha katika kuhudhuria warsha hiyo na kuwataka waendelee kuchota mafundisho ili yawe msaada kwao na kwa wengine .
“Mkawe mabalozi wazuri hasa katika hili la uchumi shirikishi wa soko jamii  ili mlete matunda kwenye Familia na taifa,”amesema.
Amewataka akinamama kuwa wabunifu kwenye mazingira waliyopo,ubunifu utakao wafanya kujijenga kiuchumi kwasababu akinamama ndio wanaoongoza kwa kufanya shughuli ndogondogo za uchumi.
Pia Askofu Lyimo amewashukuru wafadhili waliofadhili warsha hiyo  yaani shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) kutoka nchini Ujerumani,ambapo amesema pamoja na kufadhili warsha ya wanawake shirika hilo limefadhili pia semina mbalimbali kwa kushirikiana na TEC ikiwemo ya viongozi wa dini na vijana juu ya uchumi shirikishi.
Miongoni mwa mada zilizowasilishwa ni pamoja na ,Mfumo wa uchumi wa soko jamii fursa na changamoto zake.
Pia Ushiriki na nafasi ya mwanamke katika maendeleo ya uchumi wa soko jamii.
Katika miaka ya hivi karibuni wanawake wamekuwa chanzo cha uchumi katika familia na Taifa kwa asilimia kubwa kutokana na shughuli zao ndogondogo wanazozifanya kupitia sekta binafsi kama vile mamantilie,kuuza matunda na kazi zingine nyingi,lakini bado hawaonekani  kupewa kipaumbele katika kujenga uchumi,hivyo ni wakati wa akinamama kupewa kipaumbele  kutokana na uwezo walio nao na nafasi waliyonayo katika kujenga uchumi wa Familia na Taifa kwa vitendo.
Mratibu wa Miradi katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padri Chrisantus Ndaga amesema mafunzo hayo ya wanawake ni miongoni mwa Warsha ambazo TEC imeziandaa na kabla ya hapo ulifanyika utafiti uliopelekea kuandaliwa kitabu cha uchumi wa soko jamii shirikishi kilichozinduliwa na viongozi wa dini mbalimbali nchini.
Baada ya kitabu hicho kuzinduliwa imeonekana ulazimu na haja ya kutoa mafunzo haya  kwa watu wa kada mbalimbali ili wapate uwezo wa kuiendeshea uchumi wao binafsi na kujikwamuakiuchumi na kukuza uchumi wan chi.
Ndiyo maana yalianza mafunzo ya vijana sasa akina mama.
Padri Ndaga amesema wanawake walioshiriki mafunzo hayo wana nafasi nzuri ya kuchangia uchumi wa Taifa, na hapo baadae lengo kubwa ni kuyafikia makundi mbalimbali katika Maparokia na majimbo mengine ili kuwapa fursa hii juu ya uchumi wa soko jamii shirikishi, na hasa mtu wa kijijini ili aweze kuyamudu maisha kulingana na Mazingira aliyopo.
Amesema baada ya warsha hiyo lengo jingine la Baraza la Maaskofu ni kuwafikia pia akinababa na watu wenye ulemavu.
Mwalimu Ntui Ponsian ni mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT)  na miongoni mwa wawezeshaji walioshiriki kuwezesha warsha hiyo kupitia mada yake juu ya mfumo wa uchumi wa soko jamii,fursa na changamoto  zake ambapo amesema  kila mwanamke anatakiwa kusimama na kupigania mfumo mpya wa uchumi wa soko jamii shirikishi nchini kwasababu asilimia 80 ya shughuli ndogondogo za maendeleo zinafanywa na wanawake.
Bi.Gloria Kavishe Mratibu wa Program katika Shirika la Tanzania Development Trust Jimbo Kuu Katoliki  Dar es salaam na mwezeshaji wa mafunzo hayo amesema lengo kubwa la kuwashirikisha wanawake mtindo huu mpya wa kiuchumi amabao umefanyiwa utafiti ni kuhakikisha unaleta matokeo kwa mwanamke kiuchumi.
Amesema mwanamke yupo katika uzalishaji lakini kwenye mgawanyo hayumo,hivyo kuhusisha masuala ya kijamii kwenye uchumi wa soko kutaleta tija zaidi kwa jamii maskini na katika mambo yote yanayohusu mazingira ya mwanamke anapohusika katika kutunza familia na watoto ili kazi hiyo pia ithaminiwe na kuingizwa kwenye mifumo ya kiuchumi.
Kwa upande wake Mratibu wa Jinsia na Maendeleo wa Caritas kutoka Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Bi.Glady Oning’o amelipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa mafunzo hayo na kusema endapo wanawake watayashika yote waliyopewa na wawezeshaji na kwenda kuwashirikisha wenzao juu ya suala la uchumi wa soko jamii shirikishi wanawake wengi watakuwa wamefikiwa na somo hilo na kuleta mabadiliko chanya kiuchumi.
Mafunzo hayo ya uchumi wa soko jamii shirikishi yameandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania chini ya ufadhili wa shirika la Konrad Adenauer Stiftung(KAS) la nchini Ujerumani,ambapo mada mbalimbali zimewasilishwa na wawezeshaji zikiwemo ushiriki na nafasi ya mwanamke katika maendeleo ya uchumi wa soko jamii shirikishi iliyowasilishwa na Bi.Gloria Kavishe, huku Mwalim Ponsian Ntui akiwasilisha mada ya mfumo wa uchumi wa soko jamii shirikishi Tanzania, fursa na changamoto zake.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU