Askofu Rweyongeza: Wakatoliki msidanganywe na watenda miujiza





WAkristo wakatoliki wametakiwa kuwa na msimamo wa imani na kufuata kanuni na misingi ya Imani ya Kanisa Katoliki.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo Katoliki Kayanga Mhashamu Almachius Vicent Rweyongeza katika misa Takatifu ya Kumshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 10 ya Jimbo la Kayanga na miaka 10 ya Uaskofu wake.
Misa  hiyo iliyoambatana na uzinduzi wa nyumba ya Kiaskofu Jimboni Kayanga.
Amesema kuwa mkristo mkatoliki kamwe hatakiwi kuwafuata wanaokuja  kuwadanganya  na kuwalaghai kwa fedha, magari na mali za kupita hapa duniani .
Mkristo anatakiwa kuwa na subira , uvumilivu pamoja na  kuwa na imani thabiti ambayo itasaidia kung’oa visiki na milima na kufuata kanuni msingi za Kanisa Katoliki.
Akofu Rweyongeza amesema kuwa ‘’Wahubiri feki huwahubiria watu tusiowafahamu,na wale wenye magonjwa sugu ambao tunawafahamu hawawafuati kuwaponya.
Wanatuletea watu feki ambao wameandaliwa  nanyi mnawafuata.
wangekuwa waponyaji kweli wangeenda kuponya kwenye hospitali zetu kuwaponya wagonjwa. Hawa wanaokuja wanajifanya wanatenda miujiza kwa jina la Yesu lakini wanashindwa kuelea juu ya maji kama Yesu, hawawezi kutenda kwa kufufua wafu kama Yesu.
Someni ishara za nyakati kwani  Yesu anasema wengi watakuja kwa Jina Lake.’’ amesema Askofu Rweyongeza.
Kwaupande wake Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga amempongeza Askofu Rweyongeza kwa kuadhimisha miaka kumi ya Jimbo, Miaka 10 ya Uaskofu pamoja na ujenzi wa nyumba ya Kiaskofu.
Amempongeza pia kwa uvumilivu  wake katika kipindi chote tangu Jimbo lilipokuwa change hadi sasa ambapo limetimiza miaka 10.
 Amewapongeza maaskofu,mapadri na  waamini kwa kudumu katika imani na mshikamano.
‘’Tunatoa hongera nyingi kwa Askofu wa kwanza wa Jimbo amevumilia uchanga wa Jimbo na sasa anaendelea vyema kuliongoza Jimbo na kwa macho tunaona mafanikio makubwa yaliyo bora na tunawashukuru watawa na mapadre wa Jimbo hili kwa mshikamano, utii kwake’’
Askofu Mkuu Nyaisonga amehitimisha kwa kusema, ‘’Nawapongeza kwa maendeleo yote yanayotambulika kwa jimbo na mkoa wa Kagera kwa ujumla, muendelee kuunga mkono jitihada za dhati kwa ajili ya maendeleo ya watu wote.
Muendelee kuwa mstari wa mbele kusimamia amani, mshikamano na ustawi wa taifa la Tanzania,’’ amesema.
Katika misa hiyo ya kusherehekea miaka 10 ya Jimbo Katoliki Kayanga na Miaka 10 ya Uaskofu na uzinduzi wa nyumba ya Kiaskofu,misa ilihudhuriwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, Askofu Desderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba, Askofu  Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki  Tanga, pamoja na Askofu Joachim Ntahondereye wa Jimbo Katoliki  Muyinga - Burundi, Monsinyori Inchi Matata Orest wa Jimbo Katoliki Kabungo- Rwanda pamoja  wawakilishi wa majimbo Jirani ndani na nje ya Tanzania .
Mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa ni Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye pia ni Mbunge wa Karagwe Innocent Bashungwa, aliyeambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe na vingozi wengine wa Serikali.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU