Dkt. Kikwete hatalisahau Kanisa Katoliki-Ridhiwani
LIKIELEKEA katika
kufanya kilele cha Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara hapo
Novemba 4, 2018, imeelezwa kuwa uwepo wa Kanisa Katoliki nchini na ujio wa
wamisionari umekuwa mkombozi wa watanzania hasa katika sekta ya elimu na afya,
ambapo familia ya Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
imeweka wazi kuwa haitalisahau Kanisa Katoliki.
|
Hayo
yameelezwa na Mbunge wa Chalinze na mtoto wa Dkt. Kikwete, Ridhiwani Kikwete,
wakati akiongea na waamini wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Kanisa
Kigurunyembe Jimbo Katoliki Morogoro, wakati wa Misa Takatifu ya Kutabaruku
Kanisa hilo.
“Babu yangu
mzee Mrisho Kikwete, ambaye kwa ufundi na utaalamu wake alioupata katika Kanisa
Katoliki, hata walipokuja watawala wa kijerumani walimuona anafaa kuwa mmoja wa
viongozi. Akachaguliwa kuwa wakili wa wajerumani katika shughuli zao pwani ya
Afrika Mashariki, hata baadaye wanawe wakasoma katika mfumo huo huo hata
wajukuu wake. Kwa mfano Jakaya Kikwete ambaye ni baba yangu mimi, amesoma
Middle School katika shule ambayo kipindi hicho ilikua inaitwa Lugoba ambayo
inaendeshwa na Kanisa Katoliki mpaka leo hii. Kwa hiyo Kanisa Katoliki lina
mchango mkubwa katika familia yangu” ameeleza Ridhiwani.
Akielezea
historia ya kuingia kwa ukristo nchini, Ridhiwani amesema kuwa Bagamoyo ina
historia kubwa katika Tanzania kwa kuwa historia ya Kanisa Katoliki inaanza na
historia ya ujio wa wamisionari waliotokea Re-union na kisha kufika Zanziba na
baadaye wakavuka maji hadi Bagamoyo walikousimika msalaba.
“Tokea
kipindi hicho kwa ushuhuda kabisa tumeendelea kuneemeka kwa Kanisa Katoliki
katika nyanja mbalimbali. Mimi mwenyewe katika historia ya maisha yetu, ni moja
kati ya familia zinazosimama mbele yenu hapa kutoa shukrani zangu kwa Kanisa
Katoliki”. Amesema.
Akitoa homilia
yake katika Misa hiyo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo amesema kuwa utakatifu wa kanisa ni lazima utokane na
wa waamini hivyo kuwataka waamini wa Parokia hiyo kujitakasa ili matumizi ya
kanisa hilo yalete maana kusudiwa.
“Jengo hili
litakuwa tu takatifu kulingana na utakatifu wa mwenendo wenu. Mkilitumia kwa
matumizi tofauti mtakuwa mmekufuru. Hivyo basi, kanisa hili litakuwa na maana
kutokana na sisi waamini tunaoingia hapa” amesema Kardinali Pengo.
Kanisa hilo
la Parokia ya Kigurunyembe limetabarukiwa na Kardinali Pengo na limetumia
takribani miaka 10 hadi kukamilika kwake ambapo mwaka 2013 Dkt. Kikwete
aliongoza harambee ya ujenzi wa Kanisa hilo iliyofanikisha kupatikana kwa Tsh.
Milioni 200, huku Dkt. Kikwete akichangia Milioni 70.
Asante Mungu kwa kufanikisha kutabarukiwa kwa kanisa letu la Bikira Maria Mama wa Kanisa.
ReplyDelete