Ask. Chengula azikwa Mbeya
Na Pascal Mwanache, Mbeya
WAZIRI wa Fedha na Mipango nchini Dkt. Philip Mpango amesema kuwa ni
jukumu la viongozi wa dini kukemea uovu uliopo katika jamii na hata viongozi wa
serikali wanaposhindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia watanzania.
Ameeleza hayo katika Misa Takatifu ya maziko ya marehemu Askofu Evaristo
Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya iliyofanyika kwenye Kanisa la Hija Parokia ya
Mwanjelwa, ambapo Dkt. Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Ponge Magufuli.
Dkt. Mpango amesema kuwa marehemu Askofu Chengula alikuwa na uthubutu wa
kukemea uovu katika jamii ya Tanzania, jambo ambalo viongozi wa dini hawana
budi kuliendeleza. Amebainisha kuwa Askofu Chengula alikuwa ni kiongozi wa
mfano kwa waamini wa Mbeya na watu wote.
“Waamini wa Jimbo Katoliki la Mbeya na wanachi wa Mbeya Mungu aliwapa
zawadi kubwa, aliyoihamisha kutoka Iringa akawaleteeni ninyi. Huyu alikuwa ni
kiongozi wa mfano. Aliwaelekeza watu kwa Mungu. Alithamini kazi kwa malengo,
sikuzoea sana kusikia mpango mkakati kanisani, lakini yeye katika jimbo lake
aliratibu mpango mkakati. Hii inaashiria ukweli kwamba ni lazima kazi ifanywe
kwa malengo”.
Aidha Dkt. Mpango amesema kuwa wananchi wa Mbeya watamkumbuka Askofu
Chengula kwa namna alivyojitola katika kuwapatia wananchi huduma nzuri za afya
na elimu bila kubagua.
Rais TEC: Muda uliyopangwa na Mungu ndiyo muda mwafaka
Akitoa homilia katika misa hiyo Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzana (TEC) ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda Mhashamu Gervas
Nyaisonga amesema kuwa muda uliopangwa na Mungu ndiyo muda mwafaka na kwamba
huzuni ya mkristo ni huzuni ya kiimani, siyo huzuni ya kukata tama.
“Huzuni yetu ina chembe chembe za furaha ndani yake. Marehemu alikuwa na
dira yake ambayo ni ‘Mungu dira yangu’. Hiyo ndiyo ilikuwa ndoto yake, kumfikia
Mungu ndiyo utimilifu wa matarajio yake. Ili kufikia lengo hilo aliyatenda
mambo makubwa mazuri kama wasifu wake ulivyoyataja” ameeleza.
Aidha Askofu Nyaisonga amesema kuwa marehemu Askofu Chengula alijiweka
na kufanikisha mikakati ya kielimu, afya, miito na taasisi mbalimbali ili
afikie dira yake, na hivyo ameikamilisha dira yake. “Tunahuzunika lakini huzuni
takatifu” amesema.
Salamu za TEC
Akitoa salamu kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),
Makamu wa Rais wa TEC ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu
Flavian Kassala amesema kuwa katika maisha yake marehemu Askofu Chengula
amejidhihirisha kuwa baba mwenye moyo wa kutumikia na moyo mkuu wa mapendo
ambapo historia yake inabaisha hayo wazi.
Ameeleza kuwa Askofu Chengula amekuwa chanzo cha furaha katika kila
jumuiya aliyoishi huku akidhihirisha upendo na huruma hata kwa wale waliokuwa
wanyonge ambapo hakusita kumgawia yeyote aliyehitaji upendo huo.
“Tutamkumbuka kwa malezi yake kwa vijana, kuwavuta waliopotoka warudi
kundini na kuungana na walio wema. Alivuta miito mingi katika upadri na utawa.
Alikuwa mwanga kwa wale waliotaka kuingia katika masiha ya ndoa. Matunda yake
sisi sote tunayashuhudia leo” ameeleza.
Aidha ameongeza kuwa aliweza kutoa matamko mazito kwa lugha nyepesi na
kusaidia kuwarudisha wengi, na kamba kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa TEC
kwani alikuwa chombo muhimu kwa umoja wa baraza. “Alikuwa tunu na hazina ya
busara kwetu sisi maaskofu” amesema.
Naibu Spika atoa ombi kwa maaskofu
Akitoa salamu za rambi rambi Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa alichojifunza kutoka kwa Askofu
Chengula ni kuwa na Upendo usio na mipaka.
“Alinipenda, nitajitahidi na nitamuomba Mungu anisaidie ili niweze
kuwapenda watu wote bila mipaka. Alikipenda sana Kituo cha Afya cha Chewa,
lakini pia sehemu ya kulelea watoto yatima, yeye alikuwa baba yao. Ninawaomba
ili watoto wale na sehemu ile iendelee kuwa kimbilio kama ambavyo Askofu
Chengula alivyopafanya kuwa kimbilio” ameeleza.
Msimamizi wa Jimbo
Wakati huo huo Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Padri Francis Magalla
kuwa Msimamizi wa Jimbo Katoliki la Mbeya, baada ya aliyekuwa Askofu wa Jimbo
hilo Mhashamu Evaristo Chengula kufariki Dunia Novemba 21 mwaka huu.
Barua ya uteuzi huo imesomwa katika misa hiyo na Balozi wa Baba
Mtakatifu nchini Askofu Mkuu Marek Solczyński ambaye pia aliongoza adhimisho hilo la Misa Takatifu.
Maziko ya Askofu Chengula
Mara baada ya mwili wa Askofu Chengula kuagwa TEC Novemba 26, 2018
ulisindikizwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na
kusafirishwa hadi Mbeya. Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Askofu
Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki la Mbeya aliyefariki dunia Novemba 21, 2018
umezikwa kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki Mbeya,
Novemba 27, 2018.
Askofu Evaristo Chengula alizaliwa Januari Mosi 1941, huko Mdabulo,
Mufindi, Mkoani Iringa. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kipadri,
tarehe 15 Oktoba 1970 akapewa Daraja Takatifu ya Upadri.
Tarehe 8 Novemba 1996, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu
wa Jimbo Katoliki Mbeya na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 2 Februari 1997.
Askofu Evaristo Marcus Chengula Amefariki dunia tarehe 21 Novemba 2018 kwenye
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini
Dar es Salaam.
Raha ya Milele umpe ee Bwana, na Mwanga wa milele umuangazie, apumzike
kwa amani, AMINA.
Comments
Post a Comment