Katibu Mkuu TEC: Wananchi msikebehi maelekezo ya serikali dhidi ya corona
JAMII imetakiwa
kutokuzikebehi na kuzibeza juhudi
zinazofanywa na serikali katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa
hatari wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, badala yake itekeleze
kwa vitendo maagizo na miongozo inayotolewa.
Rai hiyo
imetolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri
Charles Kitima katika mahojiano maalum na vyombo vya Habari nchini,
yaliyofanyika katikati ya juma ofisini kwake Kurasini jijini Dar es Salaam.
Amesema,
Kanisa Katoliki nchini linaridhishwa na hatua zinazofanywa na serikali kupitia
Wizara ya Afya katika mapambazo dhidi ya ugonjwa huu ulionea sehemu mbalimbali
duniani, hivyo akasisitiza kwamba hakuna sababu ya baadhi ya watu ama makundi
ya kijamii kuzibeza na kuzikebehi juhudi hizo.
Katika
kusisitiza zaidi amesema “Tuiache Serikali ifanye kazi yake kwa kutumia
wataalam wa afya iliyonao na kila mmoja kwa nafasi yake, atoe ushirikiano kama
inavyotakiwa…hili siyo tatizo la kukebehi wala kufanyia mzaha kwani linagusa afya za wananchi,”.
Ili
kudhibiti zaidi kasi ya maambukizi, Padri Kitima amesisitiza kila mwananchi
kujilinda mwenyewe na kuwa mlinzi wa
mwingine hasa kwa kukubali kuchukua hatua kama inavyoelekezwa na wataalam wa
afya mojawapo ikiwa ni matumizi ya
vitakasa mikono na kuwahi hospitalini pale mtu anapohisi mabadiliko ya mwili
hasa mafua yenye kuambatana na homa kali na dalili nyinginezo.
Hata
hivyo licha ya kukiri kuwa Tanzania haiko vibaya sana kitakwimu katika kasi ya
maambukizi ya covid-19 hasa kutokana na
hatua zilizochukuliwa, lakini ameishauri serikali kuendelea kusimamia na
kuiboresha miongozo hiyo ili ilete matokeo chanya zaidi.
Kuhusiana
na taarifa ya kimtandao iliyotolewa hivi karibuni kutoka Shirika la Afya
Duniani (WHO) na kuripotiwa na Gazeti la Washington Post la nchini Marekani,
kwamba katika kipindi cha wiki mbili zijazo yaani kuanzia April Mosi, 2020,
kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu barani
Afrika itaongezeka zaidi sababu kubwa zikitajwa kuwa ni ukaribu uliopo
baini ya nchi za Afrika na China na ukosefu wa vipimo, lakini Padri Kitima
akawatoa hofu Watanzania kkuwa wasitaharuki kwa kupata taarifa za kimtandao,
badala yake zaidi wasikilize kile kinachosemwa na serikali yao.
“Serikali
yetu ina wataalam wa afya hivyo Watanzania tusiwe na taharuki kusikiliza
taarifa za kimtandao , badala yake tufuate mwongozo tunaopewa na serikali yetu
yenyewe kwani anayetafasiri taarifa sahihi za kiafya toka vyanzo mbalimbali ni
chombo hiki pekee,” amesisitiza.
Amesema,
kwa sasa halisi ilivyo taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zitatolewa lakini
akasema zinatakiwa kuchujwa tena kiutaalam na katika kusimamia hili, hata
serikali yenyewe tayari imetoa maelekezo
kuwa atakayetoa taarifa kuhusu corona ni Wizara ya Afya tu.
Katika
kuhakikisha inatekeleza kwa vitendo agizo la serikali, anasema Kanisa Katoliki
upande wake, tayari limechukua hatua madhubuti kudhibiti kasi ya ugonjwa huu
kwa kuweka vitakasa mikono maeneo mbalimbali kuzunguka maenneo ya makanisa,
kutokuweka maji ya baraka kwenye milango ya Kanisa, kubadilisha utaratibu wa
kukomunika pamoja na kuhakikisha benchi
za kukalia kanisani zinasafishwa kwa kutumia dawa na sabuni maalum ya kuuwa
wadudu, vitu ambavyo pia kanisa limekuwa likiwasisitiza waamini wake
wakivitumia kwenye familia zao.
Covid - 19 ni ugonjwa unayoisumbua dunia kwa sasa ambapo hadi
kufikia Aprili Mosi, 2020 takribani watu 935,197 walikuwa wameambukizwa, kati
yao 47,192 tayari walikuwa wamepoteza maisha. Katika idadi hiyo, waliyopona ni
193,989 ikilinganishwa na watu 994,016 wanaondelea kupatiwa matibabu kati yao
35,478 wakiwa mahututi.
Comments
Post a Comment