Askofu Kinyaiya awataka waamini kuwaombea viongozi wa dini


ASkofu Mkuu  wa Jimbo  Kuu  Katoliki Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya amewataka  waamini na wote wenye mapenzi mema kuwaombea mapadri na watawa ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Wito huo hivi karibuni kwenye Misa ya kubariki mafuta ya wagonjwa, wakatekumeni na kuweka wakfu mafuta Matakatifu ya Krisma, katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Askofu Kinyaiya amesema kuwa mapadri ambao ndio wapakwa mafuta matakatifu wanapaswa kutambua kuwa wao ndio wateule wa Bwana wanaofanya kazi maalumu ya kutoa huduma katika Kanisa Mahalia.
‘’Ndugu zanguni mapadri na watawa nyie ndio mliopewa jukumu la kuwahudumia wana wa Mungu katika Kanisa hivyo mnapaswa kutenda yaliyo mema na ya kuwapendeza waamini mahali.
Katu msifanye kazi ya Kanisa kwa ubaguzi. Tendeni kwa haki kwa kila mmoja atakayehitaji huduma ya kiroho,” amesema Askofu Kinyaiya.
Pia akizungumzia jinsi Mafuta Matakatifu ya Krisma yanavyochanganywa kuwa mafuta Matakatifu ya Krisma ni mafuta ya mizeituni ambayo huchanganywa na manukato yenye gharama kubwa ambayo ina harufu nzuri na kila mpakwa mafuta hayo anapata harufu harufu ya Mwenyezi Mungu.
“Ninyi mliopakwa mafuta Matakatifu ya Krisma Takatifu tambueni kuwa kila mpitapo harufu inayotoka ni harufu ya Kristo Yesu ambaye ndiye aliyewatuma kuhubiri neno la Mungu kwa waamini mahali hivyo matendo na yote mfanyayo yawe ni kwa sifa na utukufu wa Mwenyezi Mungu,” ameongeza.
Akizungumzia mafuta ya wagonjwa Askofu Kinyaiya amesema kuwa mafuta hayo yanampa mgonjwa matumaini, faraja  na nguvu si vinginevyo.
 Hivyo tafsiri ambayo baadhi ya watu wamekuwa wakiitoa kuhusu mafuta hayo sio sahihi.
“Kumekuwepo na baadhi ya watu wamekuwa wakitoa tafsiri kuwa mtu akipakwa mafuta ya wagonjwa huyo basi hana tena matumaini ya kuendelea kuishi hivyo marabaada ya kupakwa mafuta hayo ndio mwisho wake. Tafsiri hiyo si sahihi wala sio kweli kabisa ,” ameeleza.
Kuhusu mafuta ya wakatekumeni Askofu Kinyaiya amesema kuwa mafuta hayo hutumika katika ubatizo wa wale ambao ni wakatekumeni ambao kwa desturi huwa wanabatizwa usiku wa Pasaka.
Askofu Kinyaiya amewaongoza mapadri kurudia ahadi zao za viapo vya utii kwa Askofu Mahalia  walivyoweka wakati wakipewa Daraja Takatifu la Upadri.
Amewataka mapadri kulisoma vyema neno la Mungu na kujitayarisha kabla ya kuadhimisha Ibada Ya Misa Takatifu na kutoa mahubiri ambayo yatawawezesha waamini kulisikia neno la Mungu kulielewa na kuliishi.
Pia amewataka mapadre wa Parokia mbalimbali za Jimbo Kuu Katoliki Dodoma kuhakikisha kuwa wanashughulikia kesi zote za ndoa zilizofikishwa kwao na katu wasikubali ziwe ni tatizo kubwa na ikiwezekana wapewe zile fomu maalumu wazijaze na zipelekwe mahala husika.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI