‘Wajibu wa serikali ni kuangalia Raia wake’
ASkofu wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, Mhashamu Severine Niwe-Mugizi
ameiomba serikali kusaidia baadhi ya vituo vinavyowasaidia watoto wanaoishi
katika mazingira magumu kwenye jamii.
Askofu Niwe-Mugizi ameyasema hayo Machi 2
mwaka huu wakati akifungua bweni la wasichana katika kituo cha watoto cha
Nazareti kilichoko Nyamiaga, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera. Hafla hiyo
ilitanguliwa na tukio la kubariki vyumba vya bweni hilo.
“Watoto wanaosaidika ni wa jamii
ya Tanzania na hivi hata serikali inapaswa kufikiria pia nini inachoweza
kufanya ili kusaidia huduma ya hiki kituo ili kiendelee,” Baba Askofu
NiweMugizi huku akiongeza;
“Najua serikali ina mambo mengi sana lakini
wakishaona kwamba kituo kinasaidia watoto wa Tanzania, wataweza kutuunga mkono.
Inawasaidia hata wao kwa sababu ni wajibu wa kwanza wa serikali kuwahudumia
hawa watoto.
Serikali ndiyo inastahili kuwa
mstari wa mbele katika kuangalia mahitaji ya raia wake na haswa watoto maana
ukishawaacha waishi maisha yasiyopendeza basi kesho unapata watoto wasio na
maadili, walio wakorofi.”
Aidha, amewahimiza wazazi wa watoto hao
kushirikiana na Masista hao ili kuwatunza hawa watoto.
“Wazazi wakifundishwa kwamba kufika hapa
kituoni na kumsalimia mtoto kunajenga uhusiano ambao ni wa kibinadamu ni muhimu
sana. Hata kama huna rasilimali za kumtunza, mtoto ataona kwamba unampenda,”
ameeleza.
Pia
amewahimiza watoto kuwa na nidhamu na kuwapenda walezi wao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika hilo Barani
Afrika, Sista Christiane Lapierre ameshukuru Mungu kwa mafanikio hayo.
Ametaja baadhi ya changamoto
wanazokumbana nazo mojawapo ikiwa ni upungufu wa misaada kutoka kwa wafadhili
na kupata wakati mgumu wa kuendesha kituo.
“Tangu zamani tulitamani kupokea watoto
wasichana, na sasa tumefanikiwa na ni furaha kubwa kwamba tumejenga nyumba yao
ya kuishi.
Tunamshukuru Askofu Severine kwa
kuja kubariki jengo hili. Asante kwa masista wote waliojitoa wakati wa ujenzi,”
amesema =Sista Lapierre wakati wa hotuba yake.
Mmoja wa watoto wanaolelewa kituoni hapo
ambaye pia ni wanafunzi wa shule ya Msingi Nyamiaga Filbert Mugisha amesema
watazidi kushirikiana na masista pamoja na wafanyakazi ili kufikia ndoto zao.
Kituo cha Nazareti kinasimamiwa na Shirika la Masista
wa Mtakatifu Christiana linalofanya
utume kwenye Jimbo Katoliki
Rulenge-Ngara. Kituo hicho kinatoa malezi kwa watoto wanaotoka katika
mazingira magumu.
Kituo hicho kilianzishwa mwaka 2012 huku
kikipokea watoto wa kiume tu, lakini baada ya kuzindua jengo hilo, sasa
kimeanza kupokea watoto wa kike wanatoka katika mazingira hatarishi.
Kwa sasa kituo hicho kinajumla ya
watoto 39 kati yao wavulana ni 28 na wasichana 11 wote wakisoma shule za msingi
ikiwemo shule za msingi za Nyamiaga, Mbinyange na Ngara mjini.
Pia wapo watoto 64 ambao
wanasaidiwa wakiwa nje ya kituo yaani nyumbani kwao lakini pia wana watoto tisa
ambao wanasoma shule za sekondari za Ndomba na Kabanga pamoja na mwanafunzi
msichana mmoja ambaye anasoma QT katika shule ya sekondari ya Lukole.
Kwa mujibu wa Askofu NiweMugizi, Jimbo la
Rulenge-Ngara lina vituo viwili vya kuwasaidia watoto wanaotoka mazingira
magumu. Kituo kimoja kinasimamiwa na Masista wa Shirika la Mtakatifu Francisko
wa Bernadetta wa Lourdi, (FSSB). Kituo cha pili kinasimamiwa na Shirika la
Masista wa Mtakatifu Theresa wa Calcutta, (M.C) vyote vikiwa kata ya Rulenge.
Comments
Post a Comment