Mbunge kuanzisha chama cha Moyo Mtakatifu wa Yesu bungeni
MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini amesema ataanzisha
tawi la chama cha kitume cha Moyo Mtakatifu wa Yesu katika Jumuiya yake iliyopo
Bungeni huku akimwomba Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya kuwa tayari
kufanya uzinduzi pindi atakapoanzisha chama hicho cha Kitume.
Amesema hayo katika kilele cha Jubilei ya
Miaka 100 ya Chama cha Kitume cha Moyo
Mtakatifu wa Yesu kiliyofanyika katika viwanja vya Hija Mbwanga Jimbo Kuu
Katoliki Dodoma.
Wakati huo huo, Spika Mstaafu wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Anna Makinda ameongoza harambee kwa ajili ya ujenzi wa
jengo la Groto ya sanamu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu na kufanikiwa kukusanya TSh
8,493,750.
Mbunge Selasini ametoa ahadi hiyo
alipopata nafasi ya kuzungumza akiwa miongoni mwa wanachama wapya 75
walipokelewa kwenye Chama cha Kitume cha Moyo Mtakatifu wa Yesu kwenye kilele
cha jubilei hiyo.
Selasini amemshukuru Spika Staafu Makinda
kwa jitihada zake za kueneza na kukoleza imani ya Kanisa tangu alipokuwa
bungeni alipowakusanya wabunge Wakatoliki na kuanzisha jumuiya ndogondogo,
ambapo na yeye alibahatika kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo bungeni.
Katika salamu zake, Selasini amesema
Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu wanapoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu
kuanzishwa kwake mwaka 1919 nchini, wasisahau jukumu kubwa walilonalo la
kukeneza chama hicho kila mahali.
“Nami naomba niungane na mwenzangu
(Makinda) kuwakumbusha kuwa, leo hii tunapoadhimisha jubilee hii ya miaka 100
tangu chama kianzishwe nchini, tusisahau kuwa jukumu kubwa tulilo nalo kwa sasa
ni kueneza chama hiki kila mahali,” amesema Selasini.
Akizungumza katika harambee hiyo Askofu
Mkuu Kinyaiya amesema ni jambo zuri waliloliwaza viongozi wa Taifa wa kuenzi
Moyo Mtakatifu kwa kujenga groto hiyo ya Sanamu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu
sanjari na kufanyia kilele cha maadhimisho hayo Jimboni Dodoma.
Amesema umefika wakati Wakristo kujiunga
na chama cha kitume cha Moyo Mtakatifu wa Yesu kwani wao ni chumvi na mwanga
kwa wengine hususani katika kukuza imani.
Askofu Kinyaiya amezungumzia pia suala la
watoto wa mitaani akisema kuwa kila mmoja
akiwajibika katika nafasi yake tatizo la watoto wa mitaani litapunga na
hata siyo kupungua litatokomea kabisa katika mikoa na majimbo yetu.
“Upendo umekuwa ukitoweka kila siku ndani
ya familia zetu, ugomvi, mafarakano, mapigano, uhasama, chuki, fitina vyote
hivi vinasababisha hata watoto wetu wazikimbie familia na makazi yao ya
nyumbani na kukimbilia kuja kuishi mitaani ambako wanazidi kuharibika zaidi
kwani wanakosa hata malezi ya wazazi,” amesema
Akaongeza: “Hakikisheni kuwa mnakuwa watu
wa kufundisha na kurekebisha tabia za watoto na vijana wenu ili wabadilike
kwani wakibadilika hata magerezani kutakuwa hakuna wahalifu na ni mategemeo
yangu kuwa siku moja magereza yote yanakuwa hayana wahalifu ili tuyabadili yawe
ni madarasa kwa ajili ya watu kusomea.”
Askofu Kinyaiya amesema wakati mwingine Wanamoyo na
Wakatoliki wamekuwa waoga wa kushauri wanapomuona mtu anafanya au kuelekea
kufanya vibaya kwa kumuonea aibu jambo ambalo siyo sahihi.
“Usimuonee aibu mwambie, mpashe tu na
ndiyo maana Moyo Mtakatifu wa Yesu umefunguliwa pale, mlango umefunguliwa na
sisi tumepata nguvu hiyo tuitumie tuifanyie kazi,” amesema.
Akizungumzia suala la ndoa amesema kuwa,
upendo wa kweli unahitaji sadaka, hivyo amewataka wanandoa hususani vijana
kulitambua hilo, kwani kundi lao ndilo linaloongoza na kuathiriwa kwa kukosa
upendo na kuvumiliana.
“Sasa ndugu zangu na hasa nyie vijana wale
walio na hizi ndoa freshi freshi hilo kwao ni taabu kweli, wakikoseana kidogo
toka hapa kwenda kwa mama yako!” ameeleza.
Awali akizungumza juu ya ujenzi wa groto
hiyo, Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, Longinius
Kagaruki amesema itagharimu Sh 7,000,000 lakini kwa kuwa tayari ipo pia groto
ya Mama Maria pembeni ya watakapojenga groto ya sanamu ya Moyo Mtakatifu wa
Yesu itabidi iboreshwe kwa kuwekewa mazingira mazuri kwa ajili ya watu kusali
kwa utulivu zaidi.
“Kwa kweli groto ya Mama Maria imejengwa
vizuri, ila mazingira ya watu kukaa na kusali hayapo vizuri, hivyo tumeona ni
bora tuyaboreshe ili watu waweze kusali kwa utulivu na kwa kutafakari kwa kina
sala na maombi wanayokuwa nayo,” amesema Kagaruki.
“Groto ya sanamu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu
itagharimu kiasi cha shilingi milioni saba tu na shilingi milioni tatu nyingine
ndizo zitatumika kuboresha mazingira ya groto ya Mama Maria,” amesema.
Kwa mujibu wa Kagaruki, tayari Askofu Mkuu
Kinyaiya ameshawapa eneo na kuwaonesha mahali ambapo watajenga groto hiyo itakayokuwa ni alama ya miaka 100 ya chama
hicho tangu kianzishwe.
Viongozi hao wamesema sanamu itakayowekwa
kwenye groto hiyo imenunuliwa Sh milioni 2 kutoka katika duka kubwa la
visakramenti la
Jimbo Kuu Katoliki Dodoma lililopo katika
Parokia ya Mtakatifu Petro Swaswa.
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Mungano
wa Tanzania, Anna Makinda, amewashauri Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu nchini,
kushuka hadi ngazi ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo kueneza chama hicho.
Mama Makinda ametoa ushauri huo wakati
akitoa salamu kwa wanachama wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, baada ya Ibada ya Misa
Takatifu ya Kilele cha Jubilei ya Miaka 100 ya chama hicho kitaifa,
iliyofanyika jimboni Dodoma.
Makinda ambaye pia ni mwanachama wa chama hicho
cha kitume, amesema ipo haja kwa wanachama hao wa Moyo Mtakatifu wa Yesu
kujizatiti katika kukieneza chama hadi ngazi ya chini ya Kanisa hususani
jumuiya Ndogondogo za kikristo, ili waamini mahalia watambue umuhimu wa kufanya
ibada na kutoa heshima kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Amesema wao kama wanachama wanapopeleka
ujumbe katika jumuiya, baadhi ya waamini hasa vijana hushangaa kukiona na
kukisikia chama hicho, akitolea mfano katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam
anakotoka yeye.
“Naomba nitumie nafasi hii pia kuwashauri
wanachama wenzangu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu mliopo hapa, twendeni tukakieneze
chama hiki hadi kwenye jumuiya ndogondogo za Kikristo ili watu watambue na
kujua umuhimu wake ni nini,” amesema.
Moyo Mtakatifu wa Yesu... Ufalme wako ufike...
ReplyDeleteHongera sana Mhe. Mbunge Joseph Selasini. Moyo huo ukawe chachu kwa wengine wengi ili wavutiwe na moyo Mtakatifu wa Yesu na kujiunga kwa wingi katika utume huo ili kueneza ibada na kuuhesgimu moyo Mtakatifu wa Yesu uliojaa mapendo kwetu wanadamu. Wote tunaalikwa kuukimbilia na kuutuliza moyo Mtakatifu wa Yesu.