Askofu Banzi aadhimisha jubilei miaka 25 ya Uaskofu
ASkofu wa Jimbo Katoliki Tanga Mhashamu Anthony Banzi
ameadhimisha jubilei ya fedha (miaka 25) ya uaskofu.
Maadhimisho
ya Jubilei hiyo yamefanyika hivi karibuni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu
Anthony wa Padua Chumbageni Jimboni humo.
Papa Fransisko amemtumia
Salamu za pongezi Askofu Banzi akisema anamshukuru Mungu kwa kulitumikia Kanisa
katika Jimbo Katoliki Tanga.
Akisoma
salamu hizo kwa niaba ya Baba Mtakatu, Balozi wa Baba Mtakatifu Nchini Askofu
Mkuu Marek Solczyn’sk amesema kuwa, Papa anampongeza Askofu Banzi kwa utume uliotukuka
katika Kanisa la Tanzania na hasa Jimbo la Tanga. Anamuombea baraka za Mungu
aendelee kuchunga kondoo wa Mungu na kulikuza Kanisa jimboni Tanga.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC limempongeza Askofu Banzi kwa utume
uliotukuka huku likimuombea na kumshukuru kwa kujitoa kwa moyo bila kuchoka kwa
muda wa miaka 25 ya uaskofu wake.
Akiwakilisha
salamu hizo za TEC Makamu Mwenyekiti wa
TEC Askofu Flavian Kassala amesema kuwa,
Baraza linamshukuru Mungu kwa zawadi ya Askofu Banzi katika Kanisa la Tanzania.
Pia
linamshukuru Askofu Banzi kwa kuitikia wito
wa Upadri hatimaye uaskofu.
Amesema
kuwa, Askofu huyo amejitoa kuwadumia masikini
na watanzania bila kuchoka zaidi wanamuombea afya njema aendelee
kumtumikia Mungu kwa sadaka zake.
“Baraza
la Maaskofu linatambua kuwa safari ya kichungaji kwa muda wa miaka 25 siyo
rahisi hata kidogo kwani umepitia vipindi vyote ya uchungu na furaha.
Hivyo Baraza linakushukuru kwa kuweza kujitoa na
kutumika bila kuchoka, kufanya kazi ndani ya baraza na hata nje ya Taifa kwa
lengo la kumuhubiri Kristo.
Tunakuombea kwa Mungu aendelee kukushika mkono katika
safari nyingine ya kulitumikia Kanisa kwa miaka mingine zaidi ili uweze kulihudumia Kanisa la
Tanzania, Afrika na zaidi sana dunia yote,” amesema Askofu Kassala kwa niaba ya
Kanisa Katoliki Tanzania.
Aidha
ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na Kanisa katika kuihudumia jamii.
Amesema
kuwa Kanisa linatambua mchango wa
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
inavyoendelea kutoa ushirikiano na Kanisa Katoliki huku ikiendelea
kulinda Uhuru wa kuabudu.
Pia
Linatambua jitihada za Rais John Pombe
Magufuli kwa kushirikiana na Kanisa Katoliki katika masuala mbalimbali bila
kuchoka.
“Zaidi
sana leo tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Magufuli
kwa kujitoa kumuhudumia Askofu Mkuu wa
Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Askofu
Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi tangu
alipokuwa mgonjwa kule KCMC hadi aliposafirishwa kwenda Hospitali ya Tiba ya
Mifupa MOI akapatiwa matibabu na sasa hali yake inaendelea kuimarika.
Tunamshukuru
sana kwa majitoleo hayo na tunakuomba Mh. Ummy Mwalimu upeleke salamu na
shukrani zetu kwa Rais kwani tumefarijiwa na ushirikiano wake huo,” amesema.
Amehitimisha
kwa kusema kwa ushirikiano wa serikali na Kanisa Katoliki utaendelea kulinda
tunu ya haki za binadamu kwani kulinda
tunu hizo hakuna utengano wa itikadi za dini, kabila au vyama vya siasa bali ni
wajibu wa wote.
Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar
es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amempongeza Mhashamu Banzi kwa
kuadhimidha Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wake Septemba 15, mwaka huu na
kumtaka asikate tamaa kwa mazingira magumu na changamoto alizopitia na
atakazopitia kwani ni sehemu ya maisha ya uchungaji.
Kadinali
Pengo amesema licha ya mafanikio katika utume wake, pia zimekuwepo kauli na
changamoto mbalimbali zilikaribia kumkatisha tamaa, lakini Mungu ameendelea
kuwa pamoja naye katika safari ya kuliongoza kundi lake.
Amemkumbusha
Askofu Banzi kuwa, miaka 25 ya uaskofu haipaswi kuwa kituo cha kupumzika, bali
kiwe mwanzo mpya wa kuendelea na safari yake ya kiimani hadi Mungu atakapomuita
hivyo, aendelee kumuomba Mungu amjalie afya na kuliombea Jimbo la Tanga na
Kanisa kwa ujumla.
Kwa
upande wake, Askofu Banzi amewashukuru viongozi wa serikali, maaskofu, mapadri,
watawa wa kike na wa kiume, waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwa
kushirikiana naye kwa kila hatua ya maisha yake zaidi sana katika miaka ya 25
ya uaskofu wake.
Amesema
kuwa, anafurahia wito wake kama Askofu na hata angeambiwa aanze leo kuchagua
wito wa maisha yake, wito wake ni upadri.
“Ninapenda
wito wangu na ninamshukuru Mungu kwa ulinzi wake hadi kufikia hapa.
Ninawashukuru wazazi wangu, ndugu jamaa na marifiki kwa kunilea na kuniingiza
katika imani hii.
Ninawashukuru
wanadarasa wote kuanzia shule za msingi, sekondari, seminarini na mapadri wote
kwa ushirikiano hadi nimefikia siku hii.
Zaidi
sana niwashukuru Maaskofu wenzangu kwa ushirikiano wa dhati kuanzia ngazi ya
Baraza kwani kupitia sala zenu na ushirikiano nimeweza kufika hapa,” amesema
Askofu Banzi.
Amemshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania John Pombe Magufuli jinsi
anavyo pambana na ufisadi na kufunga mianya ya rushwa na kuendelea kuboresha
huduma mbalimbali za kijamii na kufungua njia za kiuchumi.
“Tunashuhudia miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi ukiwemo ujenzi wa
reli ya kisasa ya Standard Gauge, miradi mikubwa ya umeme na mradi wa bomba la
mafuta kutoka nchini Uganda hadi Tanga, kuboresha usafiri wa anga kwa kununua
ndege za kisasa na kuboresha miundombinu ya barabara na huduma nyingine za
maendeleo ya kijamii.
Kwa
hayo yote yanayotekelezwa na serikali, si kwamba Kanisa Katoliki Tanzania na Jimbo Katoliki
Tanga tunakuwa watazamaji tu, la hasha!
Tunashiriki kikamilifu kuibua na kuinua
yale ambayo yanahitajika kwa watanzania wote kwani Viongozi wa Kanisa wana
wajibu wao kiroho na kimwili,” amesema Askofu Banzi.
Waamini
mbalimbali wa Jimbo Katoliki Tanga wamesema kuwa, Askofu Banzi katika miaka
yake 25 ya kuliongoza Jimbo Katoliki Tanga, kumekuwa na kukua kwa imani hasa
kwa waamini kupokea na kuishi sakramenti mbalimbali.
Mengine
wanayofurahia wamesema ni ongezeko la vituo vya afya, ukuaji wa miito
mbalimbali, ongezeko la mashirika ya kitawa ya kike na kiume, kuboresha na
kukuza sekta ya elimu kwa kuanzisha shule za chekechea, sekondari na vyuo
mbalimbali.
Comments
Post a Comment