Maaskofu wataka mapadri kutoa mahuribi hai si vijembe
RAis wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya,Mhashamu Gervas Nyaisonga
amewataka Wahubiri wa Neno la Mungu
kuzingatia kanuni bora za utoaji mahubiri yao kwenye maadhimisho mbalimbali
ya Liturujia.
Ameyasema hayo wakati anafungua Warsha ya Uboreshaji wa kutoa Homilia iliyofanyika
kwenye Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania iliyowakutanisha wajumbe wapatao 60
toka majimbo 26, wakiwemo Manaibu wa Maaskofu kutoka majimbo 15.
Askofu
Nyaisonga amewaambia washiriki hao kuwa, waamini wanaguswa sana na
mahubiri yanayotolewa kanisani,hivyo ingawaje ni ya muda mfupi yanahitajika
sana ili kuwatia moyo wakristo wanaoyasikiliza.
Kwa mujibu wa Askofu Nyaisonga Ibada
mbalimbali zinazoongozwa na mapadri zinapaswa kuwa hai na kwamba uhai huo
unachangiwa na mahubiri ya adhimisho husika.
“Mahubiri yenu yasidorore wala yasikinaishe
wasikilizaji kwa sababu yakiwa hivyo hayatakidhi lengo la Uinjilishaji,”
amesisitiza Mhashamu Nyaisonga.
Katika kufikia malengo hayo amewahimiza
Mapadri hao wakiwemo Waratibu wa Liturujia
pamoja na Wakurugenzi wa Uchungaji Majimboni, kujiandaa vizuri kwa kusoma machapisho mbalimbali na kuzingatia
sala wakati wa kuandaa mahubiri yao.
Mapema akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC, Naibu Katibu Mkuu WA TEC Padri
Daniel Duwe amewakaribisha washiriki wote katika Makao Makuu ya Baraza na
kuongeza kuwa fursa ya Warsha hiyo itaboresha mawasiliano baina ya Baraza na
Majimbo kwa kuwa inawakutanisha Viongozi wa Kanisa ambao hukutanika kwa nadra
sana.
Kwa upande wao Katibu Mtendaji wa Idara
Padri Paul Chiwangu na Askofu Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia,Mhashamu Askofu
Salutaris Libena waliwakaribisha wajumbe waliohudhuria Warsha hiyo ambayo
iliongozwa na mada zilizotolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba
Mhashamu Method Kilaini na Askofu Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara amabye ni
Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia katika Baraza.
Mada ya kwanza ilitolewa na Askofu Libena
ambaye alizungumzia juu ya Homilia, tafsiri ya Liturujia kadiri ya Hati ya
Mtaguso wa Pili wa Vatikano pamoja na nafasi ya Liturujia katika maadhimisho ya
fumbo la Ekaristi.
Wakiwa wanashirikishwa kazi za Kikuhani za
Kristo,wahubiri wanapaswa kufuata nyayo za Kristo aliyelihubiri Neno la Mungu
pale aliposema: “Tubuni na kuamini na kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.”
Katika hali hiyo mapadri hawana budi
kulipatia heshima na uzito wa pekee Neno la Mungu kwa sababu Yesu yumo ndani
mwake.
Ukiondoa uwepo wa Kristo katika Neno, yumo
pia katika Ekaristi na katika Sakramenti zote.
Kristo yupo pia katika watumishi wake
sanjari na kwenye jumuiya kutokana na kauli yake aliyosema: “Wakutanikapo
wawili au watatu kwa jina lake, yeye yupo katikati yao.”
Amehitimisha mada yake kwa kuwakumbusha
washiriki lengo la kila adhimisho la
Kiliturujia;yaani Mungu anatukuzwa na wanadamu wanapata wokovu wao.
Mada ya pili ilitolewa na Mhashamu Askofu
Kilaini ambaye alijikita kuzungumzia juu
ya Mwongozo wa Mahubiri katika adhimisho la Kiliturujia.
Alieleza kuwa msingi wa huduma hiyo ni Yesu
mwenyewe aliyewaagiza mitume wake na waandamizi wao: “Basi enendeni mkawafanye
mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho
Mtakatifu na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi”(Mt.28:19-20).
Katika kuzingatia hilo ndio maana hata Papa
Fransisko katika barua yake ya Kichungaji
aliyoiita “Evangelii Gaudium” anasema kuhubiri ni mojawapo ya vipaumbele
katika maisha ya Kanisa.
Kwa muhtasari Papa huyo amesisitiza umuhimu
wa kila Mhubiri kujiandaa ipasavyo kabla hajapanda mimbarini kuhubiri.
Kwa mujibu wa Kiongozi huyo wa Wakatoliki
duniani Mhubiri asiyesali na kujiandaa kwa ajili ya mahubiri yake si makini na
hawajibiki na amemwita nabii mwongo.
Askofu Kilaini aliwakumbusha wahubiri wote
kuzingatia hatua muhimu zinazotakiwa kufuatwa wakati wa kuandaa mahubiri na
wakati wa kuhubiri kwenyewe.
Aidha,mahubiri yajengwe katika Neno la
Mungu na si vinginevyo.
Aliwaasa kutotumia mimbari kwa kujihubiria
wenyewe kwa majigambo mbalimbali au kuwakemea wakristo bila sababu za msingi.
Pia mhubiri asitumie muda wa mahubiri kwa
kutoa utetezi dhidi ya tuhuma zake(zikiwepo),kuwasema watu,vijembe au kila
Dominika kurudia neno lile lile alilolisema siku za nyuma.
Alihitimisha mada yake kwa kuwakumbusha
wanawarsha kuwa mahubiri ni sehemu ya Liturujia na ni Ibada.
Mahubiri yaguse mahitaji ya wasikilizaji
kusudi yamjenge kiroho na kimwili na hatimaye achukue hatua.
Kwa kuwa mahubiri ni sehemu ya Ibada
inahimizwa,sehemu hiyo iongozwe na
Hiarakia na kama Mlei ana jambo la kuwaambia wakristo wenzake litafutiwe
nafasi nyingine badala ya kipindi cha mahubiri.
Baada ya maswali na majibu mbalimbali
yaliyohusu Liturujia,yalitolewa Maazimio mbalimbali kutokana na mada
zilizozungumziwa.
Kisha Askofu Libena aliwashukuru wajumbe
toka majimbo yaliyohudhuria warsha hiyo ya aina yake na kwa namna ya pekee
alimshukuru Katibu Mkuu wa Baraza aliyetafuta fedha kwa ajili ya mafunzo hayo.
Kabla hajamaliza shukrani zake alimpongeza
na kumshukuru Mhashamu Askofu Kilaini kwa utayari wake wa kuja kutoa mada
kwenye mkusanyiko huo uliowakutanisha Manaibu wa maaskofu, wakurugenzi wa
uchungaji na waratibu wa Liturujia majimboni.
Majimbo yote Katoliki yalituma wajumbe
isipokuwa majimbo ya Bukoba, Geita, Ifakara, Kondoa, Mahenge, Mpanda, Singida
na Sumbawanga.
Kabla hajatoa Baraka za kufungia warsha
Askofu Mwenyekiti alitangaza kifo cha Padri wa Jimbo la Ifakara Castor
Mkapila(63) aliyefariki kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisko,
Ifakara, tarehe 18 Septemba mwaka huu.
Comments
Post a Comment