Wanaume Katoliki DSM waanzisha Bima ya Afya, Maisha
Na. Philipo Josephat-Dar es Salaam
Umoja wa Wanaume wakatoliki wa Jimbo
Kuu Katoliki Dar es Salaam umeanzisha Bima ya Afya na Bima ya Maisha.
Askofu Mkuu
Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Yuda Thadei Ruwaichi
amezindua kadi za Bima hizo hivi karibuni baada ya kuhitimisha Ibada ya Misa
Takatifu siku ya wanaume katoliki (UWAKA) katika Sherehe ya Msimamizi wao
Mtakatifu Yoseph iliyofanyika kwenye kituo cha hija Pugu jiji Dar es Salaam.
Askofu Ruwaichi amewapongeza wanaume Katoliki
Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam kwa ubunifu mkubwa wa kuanzisha Kampuni ya
Bima ya Afya na ya maisha
itakayowasaidia waamini na watu katika hali tofauti za maisha yao.
Aidha
amewataka waendelee na ubunifu mbalimbali na kubuni Bima ya Elimu itakayo
wasaidia watoto wengi wanaokosa haki ya elimu.
“Bima ya
Elimu ni ya muhimu sana kwani itasaidia watoto hasa kutoka kwenye kaya masikini
kupata elimu kwa urahisi na uhakika.
Endapo UWAKA mtafanikisha hili
linaweza kustaajabisha watu na taifa,” amesema.
Kwa upande
mwingine, Askofu Ruwaichi ameonesha kutoridhishwa na ushiriki wa wanaume katika
jumuiya Ndgondogo za Kikristo.
Amesema tangu afike katika Jimbo Kuu Katoliki
Dar es Salaam na kuzitembelea jumuiya ndogo ndogo amekutana na changamoto ya
wanaume kutohudhuria kwenye Jumuiya ndogondogo
na kusema kuna haja ya kuchukua hatua ili kukomesha tatizo hili kwa
wanaume.
Amewataka
wanaume wakatoliki (UWAKA) kubadilika na kuwa watu wa kuhudhuria Jumuiya
ndogondogo za Kikristo ili kuimarisha Kanisa.
Amesema kuna
haja ya kuchukua mawasiliano ya simu ili pindi inapofika ijumaa
wakumbushwe kuhudhuria ibada za jumuiya.
Aidha katika
homilia yake kwa wanaume wote wakatoliki waliohudhuria ibada hiyo na
kusindikizwa na akina mama na watoto Askofu Ruwaichi amesema ukimwacha Bikira
Maria Mtakatifu Yosefu ndiye Mtakatifu maarufu zaidi kuliko wote na ili mtu
aweze kuyajua haya hanabudi kuyapapasa Maandiko Matakatifu.
Amesema
kuwa, Mtakatifu Yoseph kama baba wa Familia Takatifu alikuwa mtu wa haki hivyo
akina baba wote wanatakiwa kuwa watu wa haki kama alivyo somo na msimamizi wao.
“Haki ni
kumpa kila mmoja mastahili yake, Mt.Yoseph alikuwa mtu wa haki, je wewe baba,
mtawa, ni mtu wa haki? Mungu anayomastahili yake kwetu, ametuumba, anatutawala,
ana haki ya kutumikiwa na kuheshimiwa ni katika namna hiyo tunampa Mungu
mastahili yake,” amesema.
Askofu
Ruwaichi amewataka wanaume wajue kuwa wao ni muhimili katika Taifa hivyo wanapaswa,
kulilinda na kulitegemeza Kanisa kwa vipaumbele vilivyopo sanjari na mumwombea
Baba Mtakatifu aliongoze vema Kanisa na kuliombea Jimbo.
Mtakatifu
Yosefu ni msimamizi wa wanaume wakatoliki wote, hivyo kila mwaka wanaume wa
Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam
huadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya somo wao katika viwanja vya hija Pugu na
kwa mwaka huu ibada imeongozwa na Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki
La Dar Es Salaam Mhashamu Yuda Thadei Ruwaichi na Askofu msaidizi Eusebius
Nzigilwa wa Jimbo hilo pamoja na mapadri na watawa na wa kike.
Comments
Post a Comment