Viongozi wa dini watakiwa kulinusuru Taifa
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Maridhiano
Tanzania Alhaji Ibrahim Molel amewataka viongozi wa dini kulisaidia taifa
katika kuliletea maendeleo ya kiuchumi, badala ya kutofoautina na kupigana
vijembe.
Alhaji Molel amewataka viongozi hao kuwa na umoja
pamoja na kuvumiliana katika imani ili waweze kusonga mbele na hatimaye
kuliwezesha taifa kufikia malengo yake ya uchumi wa viwanda.
Mwenyekiti huyo amesema hayo wakati alipokuwa akifungua kikao cha elimu
elekezi na namna ya kuongoza katika mikoa
na wilaya na jinsi ya kueneza maridhiano
kwa kila eneo kwa viongozi kutoka madhehebu mbalimbali ya dini waliotoka
mikoa ya Tanzania Bara kilichofanyika
jijini Dodoma hivi karibuni
Amesema kuwa viongozi hao badala
ya kupigana vijembe na kushindwa kusameheana watumie muda huo kwa ajili ya
kujenga nchi kwa ajili ya maendeleo ya
kiuchumi yatakayofaidisha kila mtanzania hapa nchini.
Akizungumza kwenye kikao hicho
amewataka viongozi hao pia kuwa na mioyo ya upendo na amani huku wakivumiliana
ili waende kwa pamoja na kudumisha amani iliyopo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Maridhiano Tanzania Mchungaji Oswald
Mlaya amewataka viongozi hao kutojihusisha na siasa badala yake wajikite kwenye
kuiombea nchi na uchaguzi ujao wa viongozi wa serikali ya vijiji mitaa na
vitongoji unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
“Kama viongozi wa dini kujiingiza
kwenye siasa na kama mnavyoona kwa baadhi ya nchi za wenzetu wanavyouana wakati
sasa umefika kwa viongozi hao kuja kwa pamoja madhehebu na dini zote kuwa na
kauli moja itakayotufanya tusipoteze
amani na umoja uliopo nchini kwetu” amesema.
Naye Mwenyekiti wa jumuiya ya
maridhiano mkoani Dodoma Shekhe Abbakari
Omary amesema, “Kimsingi chombo
hiki kwa wakati tulionao ni muhimu katika nchi yetu hivyo niwataka watanzania
kujiunga kuwa mwanachama .
Nchi yetu inahitaji malezi ya
kiroho na hakuna mahali panapoweza kupatikana isipokuwa kwenye vyombo vyetu vya
dini ikiwemo makanisa na misikiti ili tuwe pamoja. Tumeanzisha jumuiya
itakayotuweka pamoja kwa lengo kudumisha amani
na kudumisha na wananchi wafanya shughuli zao,” amesema.
Comments
Post a Comment