Mpwapwa wamuomba Rais Magufuli awatembelee

Na Damasus Mtalaze, Kibakwe
Wakazi  wa wilaya  ya   Mpwapwa   mkoani   Dodoma  baada   ya  kuchoshwa  na  uharibifu wa  mazingira  katika   wilaya   hiyo  unaofanywa   zaidi  hasa  na  watu  wenye   fedha     wamemuomba   Rais  wa  Jamhuri ya  Muungano  wa  Tanzania  Mheshimiwa    John      Magufuli  afanye  ziara  wilayani  humo  ili  aelezwe   ni  kwa  jinsi  gani  wananchi  wa  wilaya  hiyo     wameshindwa    kushiriki    kuzuia    uharibifu  wa mazingira.
Wakizungumza  na  gazeti    Kiongozi  kwa  nyakati  tofauti  wananchi  hao  waliokataa  kutaja  majina  yao  wamesema  kuwa  kama  hatua  za  dharura  hazitachukuliwa  mapema  na  wizara husika ama Kiongozi  wa juu katika serikali  yaani Rais  huenda    wilaya   hiyo   ya   Mpwapwa   ikawa jangwa kutokana  na  kuharibiwa  kwa  mazingira  hata  sehemu  ya  vyanzo  vya  maji.
Uharibifu wa mazingira umeendelea kukithiri huku  serikali  wilayani  humo   ikizimaliza  kesi  nyingi  katika  mazingira  yanayotia  watu  mashaka  hasa  serikali  za  vijiji.
Wakizungumza  na  gazeti  hili  hivi  karibuni  baada  ya  kumalizika  kwa  mkutano  wa   hadhara  uliofanyika  jumapili  ya  juma  lililopita  katika  kijiji  cha  Kibakwe  na  kuongozwa  na   serikali  ya  kijiji  hicho, wananchi  hao  wamesema  kuwa  wamechoshwa  na  kilio  hicho  na  kuwa  kilio  hicho  kingesikiwa  mapema  huenda  hata  mvua  inayoumbua  isingesumbua  kwa  sababu  uoto  asili  ungekuwepo.
Wamesema  kuwa  wameamua  kumuomba  Rais  kutembelea  eneo  hilo  kuwasaidia   kwa  sababu  ya  ukimya wa  viongozi  wa  wilaya  hiyo   pamoja  na  kilio  chao  cha  muda  mrefu  cha  kuomba   suluhu   kuhusu   kuharibiwa  chanzo cha  maji   kinachoanzia   katika  kata  ya   Wotta.
Wananchi  hao  wamesema  kuwa  bila  juhudi  za  haraka  kuhusu  suala  hilo  huenda    kijiji  cha  Kibakwe  kwa  mwaka  huu  wa  2019 na  2020 kikakosa maji  kabisa kutokana  na  mvua  kutonyesha  ya  uhakika  na  chanzo   chao  kuharibiwa  na  watu  wasiowatakia  mema  wakazi  wa  kijiji  hicho  kilichopo  bondeni  mwa  milima  hiyo  ya  Wotta.
Wamesema  kuwa  viongozi  waliopo  wameshindwa   kuwasaidia na  kuwa  sasa  uharibifu  huo  umekuwa  janga  la  wilaya   huku  viongozi  wakiwa  wameshindwa  kutatua tatizo hilo .
Wananchi  hao  wamesema  kuwa  kwa  sababu viongozi  wa wilaya  na  mkoa  huo  wameshindwa  kuzuia    uharibifu  huo   ni  afadhali  Rais  aende  huko   wilayani   kujionea    hali  halisi  badala  ya  kusikia  tu  kwenye  vyombo  vya  habari .
“Acheni Rais  aje  tumwoneshe   uharibifu  wa chanzo  cha  maji  Iyenge  , chanzo  cha  maji  Kibakwe ,  ufyekaji  hovyo  katika  milima  ya  Wotta  , mlima  wa  Matuli , mlima  wa  Lugunga  ambao  ni  mlima  wa  tisa  kwa  urefu  hapa  nchini  ukiwa  na  urefu  wa  futi   2356 ,” wamesema.
Wamesema  kuwa  kama  serikali  ingekuwa  inajali  maagizo  yake  hali  hiyo isingetokea lakini  serikali imekuwa  ikiagiza  lakini  katika  utekelezaji  imekuwa  ikijhisahau  kitu  walichodai  kuwa  si  chema kwa  maendeleo  ya  nchi.
Uchunguzi  wa  gazeti   hili  pia umebaini  kuwa  hali  hiyo  isipodhibitiwa  mapema  huenda  hali  ya  utunzaji  mazingira  wilayani humo ikawa  katika  midomo  tu  huku  mapori  yakiisha bila  usaidizi  na  kuiacha  wilaya  hiyo  uchi  kwa  kuondolewa  asili  yake  ya  uumbaji.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI