Moto wateketeza nyumba ya Mapadri Walezi wa Seminari Kuu ya Segerea
Moto umeteketeza
nyumba ya mapadri majalimu na walezi katika Seminari Kuu ya Mtakatifu
Karoli Lwanga-Segerea iliyoko jijini Dar es Salaam majira ya saa nne na nusu
usiku Januari 15 mwaka 2019.
Kwa mujibu wa Gombera wa Seminari
hiyo Padri Tobias Ndabhatinya chanzo cha moto ni tatizo la umeme
lililosababishwa umeme kurudi kwa nguvu baada ya kukatika.
“Ni kawaida yetu kila jumatano jioni tunakutana ili kushirikishana
masuala mbalimbali ya maisha yetu pamoja na kazi zetu. Wakati tunaendelea
na hilo ghafla tukasikia harufu ya kitu
kinachoungua na baada ya sekunde chache tukasikia mlio kama kitu kilicholipuka.
Kumbe ulikuwa ni moto ambao umeshaanza kuwaka kwenye ghorofa ya kwanza, ambapo
kuna vyumba vyetu vya kulala. Ndipo tukasaidiana pamoja na wanafunzi kutoka nje
na kusaidia wale waliokuwa vyumbani washuke. Kisha tukawasiliana na Jeshi la
Zima Moto ambalo lilifanya kazi yake hadi kuzima moto huo,” ameeleza Gombera
Tobias.
Amesema bado thamani ya mali zilizoungua hazijajulikana ingawa moto huo
umeteketeza vyumba 14 vya mapadri hao na hakuna mali iliyookolewa katika vyumba
hivyo.
Pia ameeleza kuwa, hakuna aliyejeruhiwa wala aliyefariki katika ajali
hiyo. Amewashukuru waseminari wa
Seminari hiyo Kuu kwa ujasiri wao na
kutumia akili na nguvu kuwaokoa baadhi ya mapadri wao waliokuwa ghorofani hadi
wakafanikiwa kuwatoa salama.
Pia waseminari hao walifanikiwa kuokoa magari ya seminari hiyo ambayo
waliyasogeza bila kuyasha maana walikuwa hawana funguo hivyo waliyasukuma na
mengine waliyabeba ili kuyaweka mahali salama yasije kuungua na kuteketea kwa
moto.
Aidha amewashukuru majirani ambao waliwapa ushirikiano na wote waliofika
kuwapa pole kwa ajali hiyo.
Hata hivyo baada ya taarifa ya
ajali hiyo kufika katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, maaskofu waliweza kutembelea seminari hiyo asubuhi ya
Januari 16 mwaka huu ili kutoa pole kwa
mapadri hao wakiongozwa na gombera wa seminari hiyo, waseminari pamoja
na wafanyakazi wengine.
Akitoa pole kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC,
Makamu Rais wa Baraza hilo (TEC) Mhashamu Flavian Kassala amewapa pole mapadri
hao kwa ajali hiyo iliyoteketeza mali
zao na kuachwa bila malazi na mavazi
pamoja na mali nyingine walizokuwa nazo ambazo ni nyenzo za kufundishia.
“Kwa niaba ya TEC ninatoa pole nyingi kwenu mapadri na waseminari wote
kwa ajali hii ingawa tunamshukuru Mungu tumewakuta salama maana hili ni tuko la
kutisha.
Tumeona na tumeshuhudia jinsi moto ulivyoteketeza jengo hili lakini
tunaomba muwe watulivu wakati masuala mengine yanaendela kufanyiwa kazi na
maaskofu wenu ili mapadri wapate mahitaji msingi ya mwanadamu na mambo mengine
yanayohitaji maamuzi ya haraka,” amesema Askofu Kassala.
Pia amewapongeza waseminari wa seminari hiyo kwa moyo wa kujituma hata
wakaweza kuwaokoa mapadri kwa mbinu ambazo sinastaajabisha.
Pia kunusuru mali za seminari mfano magari kwani waseminari hao waliweza
kuyasogeza kwa kuyabeba na mengine kuyasukuma maana walikuwa hawana funguo.
Comments
Post a Comment