Baraza la Makanisa Ulimwenguni lalaani mauaji Kenya
Dr. Olav
Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika taarifa yake
kwa vyombo vya habari anasema, wamesikitishwa sana na shambulizi la kigaidi
lililotokea katika hoteli ya DusitD2 eneo la 14 Riverside Drive, Jijini Nairobi
siku ya Jumanne, tarehe 15 Januari 2019 na kusababisha watu zaidi ya 15
kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa. Baraza la Makanisa Ulimwenguni
linapenda kutuma salam za rambi rambi kwa wale wote walioguswa na maafa haya na
kwamba, linaziombea roho za marehemu zipate pumziko la milele huko mbinguni!
Kwa majeruhi waweze kupona haraka na hatimaye, kurejea katika shughuli zao za
kila siku!
|
Baraza la Makanisa Ulimwenguni, kwa mara
nyingine tena, linachukua fursa hii kulaani vikali vitendo vyote vya kigaidi
vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao. Waamini na watu wote wenye
mapenzi mema, hawana budi kujitokeza si tu kulaani vitendo hivi vya kigaidi,
bali kuunga mkono mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na
maridhiano kati ya watu na kamwe wananchi wasikubali kuvurugwa na misimamo
mikali inayofumbatwa katika chuki na hatimaye, kutumbukia katika mipasuko,
kinzani na migawanyiko isiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na
mafao ya wengi!
Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawaalika
waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali kwa ajili ya
kuwakumbuka na kuwaombea watu wote walioathirika kutokana na shambulizi hili la
kigaidi. Hiki ni kipindi cha kuonesha mshikamano wa dhati na familia ya Mungu
nchini Kenya, ambayo kwa miaka ya hivi karibuni, imeendelea kujielekeza zaidi
katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano
ndani na nje ya Kenya yenyewe! Lakini sasa, Kenya yenyewe ndiyo iliyoshambuliwa
na magaidi. Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni
anahitimisha salam za rambi rambi kwa kumwomba Mwenyezi Mungu awakirimie
wananchi wa Kenya huruma, upendo na neema, ili waendelee kujikita katika hija
inayofumbatwa katika haki na amani!
Comments
Post a Comment