Askofu Nzigilwa apongeza Utume wa Halmashauri ya Walei Tanzania
Askofu
Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mhasham Euzebius Nzigilwa
ameungana na waamini na viongozi wa Halimashauri ya Walei Jimbo Kuu Katoliki
Dar es salaam katika kuadhimisha jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya utume wao.
Akitoa homilia yake wakati wa Ibada ya Misa
Takatifu ya adhimisho hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Msimbazi centre Dar
es salaam, Askofu Nzigilwa amesema kuongezeka kwa imani nchini kumechangiwa kwa
kiasi kikubwa na uwepo wa utume wa halimashauri ya walei.
“Nia
ya Askofu Mkuu wa Jimbo hili Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo ya kutaka
kujengwe nyumba za mapadri kwaajili ya kuwasogezea waamini huduma za kiroho
kutoka kwa mapadri ilichagizwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa halimashauri ya
walei.
Na utume wao tangu mwanzo umelipa jimbo
letu nguvu ya kuinjilisha na kukua kwa imani,” amesema Askofu Nzigilwa.
Aidha ametoa wito kwa Halmashauri ya Walei
Jimbo na kwa waamini wote waliobatizwa kuendelea kuishi kitakatifu katika wito
wowote wanaoitiwa na Mwenyezi Mungu na wanao wajibu wa kuulinda.
Amesema ipo miito mingi na miongoni mwake
ni wito wa kuwa watakatifu ambao amepewa kila Mkristo mbatizwa sanjari na wito
wa uinjilishaji unaomgusa kila mbatizwa na kama Yesu alivyoagiza na kufundisha
aliposema muwe watakatifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mtakaifu,enendeni
ulimwenguni kote mkaihubiri Injili na aliposema kama Baba alivyonituma mimi,nami
nawatuma ninyi, ni wazi kuwa kwa mafundisho hayo ya Yesu kila mtu anatumwa wito
wa uinjilishaji.
“Ndugu zangu utakatifu wa maisha ndiyo silaha na nyenzo ya
uinjilishaji na maisha hayo hayo matakatifu yanafundisha zaidi kuliko mambo
tunayofundisha na kufundishwa.
Sasa ni wakati wa kila mbatizwa kujitahidi
kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu,”amesema.
Ameongeza kuwa katika kujitakatifuza na
kuyatakatifuza malimwengu ni sharti kila mmoja apambane ipasavyo na vikwazo
vitakavyomfanya asitekeleze hayo na kushindwa kuishi kitakatifu.
Amevitaja miongoni mwa vikwazo huku
chakwanza kikiwa ni watu kusikiliza na kutekeleza maelekezo ya ibilisi jambo
ambalo ni kovu kubwa linalopelekea kushindwa kujitakatifuza na kuyatakatifuza
malimwengu kwa kuishi kitakatifu.
Pia Askofu Nzigilwa amewaasa waamini na
watu wote kuacha tabia ya kuyapelekea maelekeo yao kwa wengine badala yake kila
mtu anapofanya kosa akiri kosa lake na si kutafuta kisingizio kwa wengine kama
walivyofanya Adamu na Eva kwenye bustani ya edeni walipokula tunda ambalo
hawakutakiwa kula na kila mmoja ajue anapofanya hivyo anasikiliza na kutekeleza
maagizo ya ibilisi.
“Wanadamu huona haraka makosa ya wengine
kuliko mapungufu yao wanasahau fundisho la Yesu ambalo anatufundisha kuona
mapungufu na makosa yetu wenyewe na si ya wengine na bila kujua kwamba jambo
hilo litawafanya kutokuishi kitakatifu,” amesema.
Amesema bila kusimama imara kazi ya uinjilishaji na kuuishi utakatifu
itakuwa ngumu kwasababu ni lazima kila mmoja apambane na hila za ibilisi kwamaana
utakatifu ni zawadi na ni miongoni mwa matunda ambayo Mungu ametupatia hivyo ni
wajibu wa kila mtu kuupalilia utakatifu na ni kwanamna gani atastawisha mbegu
hiyo maishani mwake.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa harimashauri
ya walei Jimbo Kuu Katoliki Dar es salam Ndg.Richard Sillo amemshukuru Askofu
Nzigilwa kwa kuwakumbusha wajibu wao na wao wanaahidi kwamba wataendelea
kuutumikia wajibu wao waliopewa kwa kushirikiana na wengine.
Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam limeadhimisha jubilei ya
dhahabu ya miaka 50 ya halimashauri ya walei kijimbo kabla ya kilele cha
kitaifa kufanyika June 16, 2019 kwenye viwanja vya Msimbazi Centre Dar es
salaam na kukusanya waamini wa majimbo yote 34.
Maadhimisho hayo yatakuwa ya kwanza tangu
kuanzishwa kwa halimashauri ya waei mnamo tarehe 24 June 1969.
Comments
Post a Comment