Sera za nchi zisipingane na mpango wa Mungu-Ask. Dallu

Na Pascal Mwanache, Tunduru
WATUNGA sera mbalimbali za nchi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa upendo na kwa kuwahusisha wadau wa sekta husika ili sera hizo sizipingane na mpango wa Mungu kwa watu wake.
Rai hiyo imetolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Songea Mhashamu Damian Dallu wakati akitoa homilia yake katika Ibada ya masifu ya jioni yaliyotangulia kusimikwa na kuwekwa wakfu Askofu Filbert Mhasi wa Jimbo Katoliki Tunduru Masasi.
Askofu Dallu amesema kuwa Kanisa linaendelea kusali na kushukuru kwa hatua zile zinazochukuliwa na kuona kama kweli hakuna sheria zinazokuwa kinzani kwa nafasi ya Kanisa ya kutoa huduma mbalimbali nchini.
“Tunaendelea kusali kwa ajili ya vituo vyetu vya kutoa malezi ya kuelekea katika huduma ya upadri na nyumba za kitawa. Naomba huko tusikanyage kanyage katika miundombinu ya hawa wanaoandaliwa kuwa mapadri. Wasipewe idadi tofauti na mwongozo wa kawaida wakaonekana wao wawe darasa la wanafunzi 25 tu, hapana. Hiyo siyo kazi ya kikundi wala mtu, wito ni wa Mungu anaita anavyotaka. Mungu hawezi akatulazimisha katika wito wetu” ameeleza Askofu Dallu.
Aidha ametoa wito kwa wale wote wanaotunga sheria wajawe na moyo wa upendo na kuleta hali ile ambayo imekuwa nguzo kubwa Kanisa Katoliki Tanzania.
“Tusali tumuombe Mungu shule zetu ambazo zinalea kuelekea kuanza kidato cha kwanza basi wapate nafasi ya kulelewa hapo ili tuwaandae. Tusiweke tu miongozo ambayo itakuwa inatufuta bila hata wadau wenyewe kuzungumza. Hebu fikiria kwa Kanisa la Tanzania nafasi alipo Askofu Mkuu Protase Rugambwa. Yeye ni mtanzania na aliundwa kwa miundombinu hii tuliyonayo Tanzania. Tunaomba tuendelee kuiimarisha miundombinu hiyo na kuikaza zaidi siyo tu kwa ajili ya Kanisa, bali upatikanaji wa elimu bora katika nchi yetu” amesisitiza.
Pia Askofu Dallu ametaka kuimarishwa kwa malezi ya mapadri kwa kusema kuwa malezi ya upadri hayapaswi kuwa ya mkato, na kwamba lazima mapadri walelewe kwa muda wa kutosha.
“Upadri siyo haki ni wito, ni upendo wa Kristo mwenyewe anatushirikisha kwa upendeleo, siyo haki. Upadri ni wa dunia nzima” ameongeza. 


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU